Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi Wilaya ya Kakonko wamekutana na kufanya kikao kilicholenga kuchagua katibu na msaidizi wake na kupitia rasimu na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo moja ya kipaumbele ni kuhakikisha watumishi wanafanya kazi mazingira salama na kuendelea kulipa stahiki zao.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la wafanyakazi, Michael Faraay, Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi lililofanyika leo Alhamisi, Januari 22, 2026 katika ukumbi mpya wa halmashauri uliopo Kanyamfisi, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kupitia rasimu na mpango wa bajeti 2026/2027 inalenga kuendelea kuboresha mazingira mazuri na yanayovutia kwa watumishi ili kuongeza hamasa ya kazi.
“Tumelenga kuendelea kutoa motisha kwa watumishi kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kazi ikiwemo uboreshaji wa miundo mbinu ya mahala pa kazi na kulipa stahiki kwa wakati ikiwemo likizo na uhamisho”, alieleza Kaimu Mkurugenzi mtendaji.
Kwa upande wake Afisa kazi mkoa wa Kigoma, Omary Zuberi amewakumbusha wajumbe wa baraza la wafanyakazi kuwa wao ni watumishi na wastaafu wa baadaye hivyo wanapokuwa kwenye nafasi zao wajitahidi kuwatendea mema wale wanaowasimamia ili kuepusha chuki baina ya watumishi na kuacha alama.
Naye Katibu wa TALGWU Mkoa, Johnson Muyombya amewahimiza Watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na uwajibikaji ili kuepusha migogoro na wanasiasa wakati huo huo kuepuka kesi zinazoondoa sifa za Utumishi wa Umma.
Bi.Crecencia Tindwa, Katibu CWT mkoa, amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii ili yale yaliyojadiliwa yatendewe haki na kuahidi kuyafanyia kazi mapungufu yatakayojitokeza mahala pa kazi.
Katibu wa TUGHE mkoa, Ngassa Chimola ameipongeza Halmashauri kwa kutekeleza sheria mbalimbali za baraza la wafanyakazi ikiwemo kufanya vikao ili kuhakikisha Halmashauri inaendelea vizuri na kutekeleza majukumu yake.
Aidha Afisa Utumishi wa Wilaya, Michael Magesa amesisitiza mshikamano wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi uendelee na kuwataka viongozi wapya waliochaguliwa kuendelea kuwatumikia ipasavyo wanaowasimamia ili kuhakikisha maslahi ya watumishi yanatekelezwa kwa wakati.
Katibu wa baraza la wafanyakazi, Bi.Hidaya Yusuph ametoa shukrani kwa wajumbe kumchagua yeye pamoja na msaidizi wake na kuahidi kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na mazingira yaliyo salama zaidi mahala pa kazi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa