Balozi wa Pamba Tanzania Aggrey Mwanri amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa kufuatilia kampuni iliyonunua kwa mkopo tani 9 za pamba katika Chama cha Ushirika Kanyonza (AMCOS) ili fedha hizo zilipwe mara moja.
Akipokea taarifa ya majumuisho ya kampeni ya pamba kuongeza tija na uzalishaji katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri Jumapili tarehe 31.07.2022, Balozi wa pamba ameagiza makampuni yatafutwe na kulipa fedha hizo mara moja.
“Tunadai kampuni ya Mbogwe and Bukombe Cooperative Union Ltd (MBCU) wastani wa tani 9 yenye thamani ya milioni 17, fedha hiyo ikipatikana wakulima watakuwa na Imani na sisi”, alieleza bwana Feniasi Raphael Damas, Mwenyekiti wa AMCOS Kanyonza.
Bwana Renatus Luneja afisa kilimo wa bodi ya pamba na mwakilishi wa Mkurugenzi wa bodi ya pamba alieleza kuwa kwa mujibu wa taratibu hairuhisiwi kununua pamba kwa mkopo kwani kampuni inatakiwa kufika na fedha taslimu na kuwalipa wakulima kituoni hivyo ni uzembe wa viongozi wa Chama cha Ushirika. Alimwomba mkuu wa Wilaya kushirikisha bodi ya pamba wakati anachukua hatua na wao watashirikiana naye kwa nguvu zote.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kakonko ndugu Saamoja Ndilaliha alisisitiza wakulima wa pamba walipwe fedha zao ndani ya siku saba. Alieleza hana mashaka na utendaji kazi mzuri wa Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa alieleza tayari aliwaita viongozi wa AMCOS Kanyonza baada ya kupata taarifa kuwa pamba imechukuliwa kwa mkopo na kufanya kikao nao hivyo ufuatiliaji wa karibu unaendelea ili fedha za pamba iliyochukuliwa ilipwe. Hata hivyo alihimiza viongozi wa AMCOS kuwaacha wakulima wachague kampuni ya kuuzia pamba yao kwani hapakuwa na haja ya kuuza pamba kwa kampuni ambayo ilikuwa haina fedha na kuacha kampuni iliyokuwa na fedha hivyo aliahidi kuchukua hatua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndaki Stephano Mhuli aliahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na balozi wa pamba Tanzania na viongozi wengine.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa