Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF imeandaa mdahalo maalum uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lengo kuu ikiwa ni kuwaunganisha wawakilishi wa makundi mbalimbali yanayopinga ukatili wa kijinsia, kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza ukatili huo katika ngazi zote za jamii.
Mdahalo huu umefanyika Jumanne, Julai 29, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Akizungumza wakati wa mdahalo huo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndg. Stephen Mabuga, alieleza kuwa wamefanikiwa kuweka mikakati thabiti ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa wito kwa washiriki kuwa mabalozi wa kueneza elimu hiyo katika maeneo yao, na kuripoti mapema dalili zozote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kwa upande wake, Bi. Modesia Selesius, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata ya Rugenge, alisisitiza umuhimu wa kuwajengea wananchi uwezo na kuondoa hofu ili wawe tayari kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na kuhimiza ushirikiano kati ya wananchi na serikali katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mwakilishi wa Kikundi cha Bodaboda kutoka Kijiji cha Kiyobera, Bw. Adam Sabuholo, ameahidi kuwaelimisha wenzake na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa na kushirikiana na serikali huku akiiomba Serikali kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu endelevu kuhusu viashiria vya ukatili na umuhimu wa kutoa ushahidi katika kesi zinazohusiana na ukatili huo.
Mdahalo huo umehudhuriwa na makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, wawakilishi wa mabaraza ya watoto shuleni, makundi ya vijana, bodaboda pamoja na viongozi wa malezi chanya ambapo washiriki walikubaliana kuwa, ushirikiano wa pamoja ni silaha muhimu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia na kujenga jamii salama na yenye ustawi chanya katika Wilaya ya Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa