UTANGULIZI.
Halmashauri kupitia Idara ya Kilimo Umwagiliaji na Ushirika imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kusimamia shughuli za Idara kama ifuatavyo; Kutoa ushauri kwa wakulima kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalam wa ugani hususan mbinu mbalimbali za kilimo katika kuvuna na kutunza mazao baada ya kuvuna, Kuungana kukusanya mazao katika vituo vya kukusanyia mazao kupitia vyama vya ushirika (AMCOS) na kuuza kwa pamoja ili kuepuka walanguzi wa mazao na Kutoa tahadhari ya uuzaji holela wa mazao ya chakula unaoweza kupelekea upungufu mkubwa wa chakula ndani ya Wilaya.
Pia tumeendelea kutoa mafunzo na kuhamasisha wakulima juu ya uhifadhi wa mazao katika mifuko bora ya kuzuia mazao kubunguliwa na wadudu, kufanya mikutano na wakulima hasa maeneo ya skimu za umwagiliaji za Katengera na Ruhwiti kuhusu utunzaji wa miundombinu na matumizi mazuri ya maji pamoja na kuandaa mashamba na vitalu mapema ili wazalishe kwa tija. Vilevile tunaendelea kushirikiana na Taasisi na Mashirika mbalimbali kufikisha huduma za ugani kwa wakulima mfano; TARI, FAO, ENABEL, WFP, UNCDF, ITC, TMA na WORLD VISION.
HALI YA HEWA.
Kwa kipindi cha robo ya nne hali ya hewa ni mvua kiasi iliyonyesha mwishoni wa mwezi Aprili na Mei mwanzoni ikifuatiwa kiangazi na baridi ya wastani inayoendelea hadi sasa.
HALI YA CHAKULA
Upatikanaji wa chakula kwa sasa ni mzuri kwani wakulima wanamalizia kuvuna mazao ya msimu huu, hata hivyo kuna dalili za kuwepo kwa upungufu wa chakula kutokana na kasi kubwa ya uuzaji wa mazao ya chakula inayoendelea kutokana na wanunuzi kununua mazao hayo kwa bei ya juu kuliko misimu iliyopita, aidha katika kukabiliana na hali hiyo Halmashauri imewaandikia barua (Kumb. Na. HW/KNK/S.40/VOL.I/58 ya tarehe 20/06/2022) Viongozi wa Serikali za Vijiji na Kata ili kuwashauri wakulima kutouzwa chakula chote kwa lengo la kuondoa hofu ya upungufu wa chakula.
HALI YA MAZAO MASHAMBAANI
4.1 MAZAO YA CHAKULA
Kwa tathmini iliyofanyika kwa robo hii, Hali ya mazao ya chakula kwa sasa inaridhisha hasa baada ya kupata mvua za wastani sehemu kubwa ya Wilaya yetu kwani zaidi ya robo tatu ya malengo ya mavuno imefikiwa licha ya mvua chache iliyonyesha ukilinganisha na misimu mitatu iliyopita.
4.2 MAZAO YA BIASHARA
Wakulima wa zao la tumbaku kwa robo hii wanaendelea na soko la tumbaku, jumla ya mavuno ni tani 165.61(165,609.05Kg) wastani wa hekta limwa ni 115.2 kwa msimu wa kilimo wa 2021/2022. Mazao mengine ni pamba matarajio ya mavuno ni tani 960 (960,000) hekta limwa ni 960, Kahawa tani 24.8 (“Parchment” tani 23.3 na Maganda 1.5, wastani wa hekta limwa ni 48) na Alizeti wastani wa tani 25 zimekamuliwa mafuta na wakulima kuuza mafuta yao wenyewe (Wastani wa hekta zilizolimwa ni 2,022.8 matarajio ni tani 2,528.5).
(Wakulima wanaendelea kukamua alizeti yao kidogo kidogo katika mashine za watu binafsi).
KAZI ZILIZOFANYIKA
Kitengo Cha Mazao
Kutoa ushauri kwa wakulima kutumia vizuri muda wao katika kilimo hasa kuandaa
mashamba mapema na kupanda mapema.
Kuwashauri wakulima Kuhifadhi vizuri chakula kilichopatikana na kuuza ziada tu
Kuanza kwa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao Kata ya Mugunzu kwa
kushirikiana na wadau wa kilimo wa Shirika la Enabel.
Kutoa mafunzo na kuhamasisha wakulima juu ya uhifadhi wa mazao katika mifuko bora ya kuzuia mazao kubunguliwa na wadudu kwa kushirikiana na wadau wa kilimo WFP.
Kufanya tathmini ya hali ya chakula na upatikanaji wake na kufuatilia hali ya soko la mazao.
Kitengo Cha Ushirika
Katika kipindi hiki Halmashauri imeendelea kutekeleza shughuli za Ushirika kwa kusimamia, kushauri na kuelekeza vyama vya msingi kutekeleza shughuli za ushirika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Ushirika nchini kwa kufanya kazi zifuatazo;
UPATIKANAJI WA PEMBEJEO.
Katika kipindi cha robo ya tatu hali ya upatikanaji wa pembejeo hasa mbolea siyo mzuri kutokana na mbolea kuuzwa kwa bei kubwa cha kati ya Shilingi 120,000/= hadi 150,000/= kwa mfuko wa kilogram 50. Bei hizo zimewafanya wauzaji wa bidhaa hiyo kushindwa kununua mbolea ya kutosha na kusababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa mbolea ndani ya Wilaya. Aidha, Mbolea zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo hazitoshelezi mahitaji ya wakulima (mahitaji kwa mwaka ni tani 1887 wakati upatikanaji ni tani 1785).
CHANGAMOTO
Baadhi kata kutofanya hamasa ya kutosha kwa wananchi juu ya upatikanaji na
uuzaji wa mbegu za alizeti katika maeneo yao na kupelekea usumbufu kwa wakulima kutopata mbegu kwa wakati na kuifuata Kakonko hali ya kuwa ilipelekwa katika Kata zote.
Uhaba wa watumishi na vitendea kazi kwa maafisa ugani, kwani baadhi ya
maeneo hakuna maafisa ugani na hivyo wakulima kutopata ushauri unaostahili
kwa muda muafaka.
Kukosekana kwa Wafanyabiashara wakubwa wa pembejeo za kilimo(Mbolea, Mbegu na Madawa) ndani ya Wilaya.
MIKAKATI
Kuhamasisha na kuwaelimisha wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame kama muhogo na viazi na kutotumia nafaka kwa matumizi yasiyo ya lazima.
Kuendelea kuomba ajira mpya kwa mamlaka zinazohusika na ajira kufikia Ikama itakayotosheleza mahitaji.
Kuwahamasisha Wafanyabiashara ndani ya Wilaya kufanya biashara ya pembejeo za kilimo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa