Wanafunzi wa shule za msingi ambao ni wenyeviti wa kamati za Tuseme shuleni pamoja na walimu wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kumudu mazingira na kupingana na ukatili dhidi ya watoto hususani wasichana wanapokuwa shuleni na katika jamii.
Akifafanua kuhusu mafunzo yaliyotolewa kuanzia tarehe 21-23 Julai, 2025 na kuratibiwa na shirika la UNICEF , Mwalimu William Stephano Kasule kutoka shule ya msingi kanyonza ambaye ni Mwezeshaji wa mafunzo ya Tuseme na Sara Radio, ameeleza kuwa lengo la mafunzo ni kupinga ukatili dhidi ya Watoto hasa wa kike ambao wamekuwa wakikatiliwa ndoto zao.
Mwezeshaji Mwalimu Kasule ameongeza kuwa washiriki wa mafunzo watatakiwa baada ya kukamilisha mafunzo kwenda kuimarisha kamati za klabu za Tuseme shuleni ambazo zitakuwa zinatumia mbinu mbalimbali kubaini changamoto ili kumlinda mtoto wa kike ambaye amekuwa akifanyiwa ukatili.
Hivyo, wanafunzi hao watakuwa na uwezo mzuri wa kutoa taarifa kwa walimu wao ambao watakuwa ni walezi wa klabu hizi kwa kusaidia kubainisha changamoto zilizopo na kuapata msaada sehemu salama pindi wanapokuwa na ukatili huu. Wengi wao wamekuwa hawajui wapi pa kupata msaada wanapokuwa na taarifa kuhusu ukatili wanaofanyiwa.
“Kupitia hili tunaamini kwamba tunaweza kuleta mapinduzi makubwa katika kusaidia watoto hawa waweze kupata elimu yao kuanzia shule za msingi, sekondari na elimu ya juu”, alieleza Mwalimu Kasule.
Sara Joshua Shaluteli, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kumuhunga ameeleza kuwa wamejifunza namna ya kuwasidia watoto wa kike kujilinda dhidi ya ukatili unaoendelea katika jamii zao na kutao rai kwa wazazi ambao bado wanashikilia vitendo vya ukatili kuacha kwani vitendo hivyo vinaathiri afya ya akili ya watoto.
Kwa upande mwingine, Aines Daniel, mwenyekiti wa klabu ya tuseme shule ya msingi Gwarama ameahidi kwenda kutoa elimu kwa wanafunzi wengine shuleni kuhusiana na elimu waliyoipata.
“Mimi kama mwenyekiti nitakwenda kuwafundisha wanafunzi shuleni ili na wao wende kuwafundisha wengine kuepuka vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii”.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa