WILAYA YA KAKONKO
TAARIFA YA VIVUTIO VYA UTALII WILAYA YA KAKONKO
Wilaya ya Kakonko ni mojawapo ya Wilaya 7 za Mkoa wa Kigoma. Makao makuu ya Wilaya yapo katika Mji wa Kakonko. Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ilianzishwa tarehe 08/3/2013, kwa tangazo la Serikali GN. 287 ya mwaka 2011. Wilaya hii ipo upande wa kaskazini mwa mkoa wa Kigoma kati ya latitudie 3.90 hadi 5.00 kusini na longitudi 30.20 hadi 31.50 mashariki. Wilaya inapakana na Wilaya ya Ngara na Biharamulo (Mkoa wa Kagera) kwa upande wa Kaskazini na Magharibi inapakana na Jamhuri ya Burundi, Kusini inapakana na Wilaya ya Kibondo, Mashariki hadi Kaskazini Mashariki inapakana na Wilaya ya Bukombe (Mkoa wa Geita).
Ukubwa wa Wilaya
Wilaya ya Kakonko ina ukubwa wa kilometa za mraba 2,219.65 na eneo lililopo ndani ya mamlaka ya Vijiji ni Km za mraba 2,041.03 na eneo la msitu wa hifadhi ni km za mraba 178.62. Wilaya ya Kakonko ina km za mraba 1,084.2 za ardhi inayofaa kwa kilimo na ardhi inayolimwa ni km za mraba 671.8 sawa na 62% ya ardhi inayofaa kwa kilimo. Aidha wilaya ina km za mraba 806.4 ya ardhi ya malisho.
Sehemu ndogo ya Wilaya ya Kakonko ni Hifadhi ya akiba ya wanyamapori ya Moyowosi (Moyowosi Game Reserve) na Msitu wa Hifadhi ya Halmashauri (Buyungu Local Authority Forest Reserve). Maeneo haya ya wanyamapori na Msitu yapo eneo lote la Mashariki kuanzia mpakani mwa Wilaya ya Kibondo hadi mpakani mwa Wilaya ya Bukombe kwa upande wa Kaskazini mashariki. Eneo linalokaliwa na watu limeambaa upande wa magharibi mwa barabara ya Kigoma – Mwanza kupitia Kakonko. Hii inaifanya 38.6% ya Vijiji vyote vya Wilaya ya Kakonko (Vijiji 17) kushirikiana mipaka na nchi ya Burundi kwa urefu wa Km 49.
2.0 Hali ya utalii
Vivutio na Fursa za Utalii zilivyopo katika Wilaya ya Kakonko
Kuona wanyama
Wilaya ya Kakonko inapakana na Pori la akiba la Moyowosi Kigosi lenye hazina kubwa ya wanyama na uoto wa asili. Ukiwa Wilaya ya Kakonko utapata fursa ya kuona hazina kubwa ya Wanyama hawa kama Pundamilia, Tembo, Twiga, Nyati, Simba, viboko, Mamba na Wanyama wadogo kama swala, nyamela, kongoni, kudu, nguruwe pori, nzohe, na samaki aina ya kamongo na kambale. Wanyama hawa ni kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na kwa wageni wanaotembelea Wilaya hii. Wilaya inakaribisha wananchi wote na wageni ambao wangependa kutembelea na kuona wanyama na uoto wa asili katika pori hili.
Eneo hili la hifadhi linaweza kufikika kwa urahisi kupitia usafiri wa barabara kutokea Kakonko mjini.
Uwindaji wa Kitalii
Pamoja na kupata fursa ya kuona wanyama, Wilaya ina fursa ya kufanya uwindaji wa kitalii kwa kununua vitalu vya uwindaji katika pori la akiba la Moyowosi Kigosi [Community Based Wildlife Management Areas (CBWMAs)]. Wilaya inakaribisha watalii wa ndani na nje ambao wanatamani kupata fursa hii ya kufanya uwindaji wa Kitalii.
Pundamilia katika pori la akiba la Moyowosi Kigosi
Maporomoko ya Nyakayenzi
Maporomoko haya yanapatikana katika mto mgembezi katika kijiji cha Nyakayenzi kitongoji cha Bizibirinzamba B. Maporoko haya ni kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na hata kwa wageni wa naofika katika Wilaya ya Kakonko kwenda kutalii na kuburudika.
Mapango ya asili
Pango la Nyabubindi [Kasanduka]
Pango hili ni la asili na lina ukubwa kiasi cha kuingia watu takribani 50 kwa wakati moja. Pango hili linapatikana katika eneo la mlima Nyamiyaga kitongoji cha Bulembo kijiji cha Nyabibuye Kata ya Nyabibuye. Pango hili ni kivutio cha utalii cha asili kwa Watalii wa ndani na wageni wanaofika katika Wilaya ya Kakonko kwenda kujionea na kufurahi.
Pango la Kikulazo
Pango hili lipo katika kijiji cha Nyakayenzi kitongoji cha Bizibirinzamba B karibu na maporomoko ya mto Mugembezi. Pango hili linaweza kuingiza watu zaidi ya 15 kwa wakati moja.
Pango la Kibika
Kitongoji cha mgembezi kijiji cha Kabare katika milima ya Kibika. Pango hili lina ukubwa wa kuingia watu takribani 20 kwa wakati mmoja. Pango hili lina vitu vya asili vinavyoashiria historia kama michezo ya bao. Pango hili ni kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje.
Pango la Ruvumela
Pango hili lipo katika kitongoji cha Ruvumela katika kijiji cha Kabare karibu na Mto Mugembezi. Awali pango hili lilitumika kama sehemu ya kufanyia ibada za asili kama matambiko kuomba mvua au hata mabalaa mengine yanayoikumba jamii yaweze kuondoka hivyo ni moja ya kivutio cha utalii.
Mahakama ya Mwanzo Kakonko
Jengo la Mahakama ya mwanzo Kakonko linasadikiwa kujengwa miaka ya 1920 wakati wa utawala wa kikoloni wa Wajerumani nchini. Jengo hili kwa sasa limekarabatiwa na hivyo kuonekana kama jipya, hata hivyo linabaki kiwa kivutio kikubwa cha utalii kwa watu kwenda na kupata simulizi zake na kujifunza mengi kutokana na historia yake.
Nyumba ya Historia ya Ufalme wa WAHA
Kama zilivyo tamaduni zingine kuwa na historia ya tawala za kifalme, Kabila la Waha wana historia ya kuwa na utawala wa kifalme [UMWAMI] kabla ya kuja kwa Wakoloni. Historia hii inapatikana katika kijiji cha Itumbiko. Historia hii imehifadhiwa na watalii wanaweza kufika kujionea zana za asili za kabila la Waha kama pinde na mishale, mikuki na tamaduni za mavazi (Mpuzu).
Nyumba ya Historia ya Ufalme wa WAHA
3.0 Fursa za Uwekezaji
Wilaya ya Kakonko imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili ambazo hazijawekewa uwekezaji wa kutosha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji ya uwekezaji mkubwa na wa ngazi ya kati.
3.1 Kilimo
Aidha Wilaya ya Kakonko imejaliwa kuwa na hali nzuri ya hewa inayowezesha uwekezaji kuwa mzuri. Ustawi na rutuba nzuri ya udongo uliopo Kakonko hustawisha mazao mbalimbali ya biashara na chakula ikiwemo Pamba, tumbaku, alizeti, mpunga, dengu, mahindi, maharage mtama, mihogo viazi na mihogo.
3.2 Mifugo
Pia mazingira rafiki pamoja na hali nzuri ya hewa inawezesha ustawi wa mifugo, kama ufugaji wa ngombe, mbuzi, kondoo, kuku, nguruwe na sungura.
3.3 Hoteli na Migahawa
Halmashauri ya wilaya ya Kakonko imeendelea kujiimarisha kwani kuna nyumba 37 kwa ajili ya kuhifadhi wageni wa kutoka ndani na nje ya Wilaya kwa wakati mmoja. Nyumba hizo ni za viwango cha kati na za kawaida ambazo zinaweza kukidhi mahitaji ya wageni wa aina mbalimbali. Aidha kuna migahawa ya kutosha na yenye kuvutia inayoweza kutoa huduma ya chakula kizuri kwa wageni mbalimbali.
3.4 Stendi ya Kisasa
Wilaya ya Kakonko ipo katika hatua za mwisho za kumalizia ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Kakonko mjini, barabara ya kuelekea Kibondo. Katika eneo la stendi kuna uwekezaji mzuri wa benki, migahawa, maduka ambayo yatatumika kutoa huduma za usafiri na bidhaa mbalimbali kwa Watalii na jamii kwa ujumla.
3.5 Ardhi iliyotengwa kwa uwekezaji
Wilaya ya Kakonko imetenga jumla ya Ekari 50 katika maeneo ya Ibuga na Kiziguzizgu kwa ajili ya uwekezaji. Hivyo hakuna usumbufu kwa mwekezaji kupata ardhi hususani kwenye shughuli za utalii.
3.5 Maeneo ya makumbusho
Wilaya ya Kakonko ina nyumba aliyowahi kuisha Mwalimu Nyerere katika Kata ya Mugunzu. Pia Kuna nyumba aliyokuwa anaishi Chifu (Chifu wa Buyungu) katika Kata ya Kakonko.
3.6 Upatikanaji wa Nishati
Kwa upande wa nishati, karibu vijiji vyote vina umeme chini ya mpango wa wakala wa umeme vijijini (REA) huku huduma za mitandao ya mawasiliano ya simu zikiwa ni nzuri zinazotolewa na makampuni nya TTCL, Vodacom, Tigo, Aitel, Halotel.
4.0 Hitimisho
Kwa ujumla fursa za uwekezaji katika Wilaya ya Kakonko ni kubwa hivyo tunawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika ili kwa pamoja kuweza kuinua uchumi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini hususani katika Nyanja za utalii.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa