Mkuu wa Wilaya Kakonko kanali Evance Mallasa amewataka Wananchi kupitia Serikali za Vijiji kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kilimo cha kibiashara kwa lengo la kukuza Uchumi wa eneo husika na Uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Serikali za Vijiji zikae na kutenga maeneo ya uwekezaji kisha Serikali italeta miradi na kujenga miundo mbinu”, alieleza Col.Mallasa.
Katika ziara ya kusikiliza kero za Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi aliyofanya Mkuu wa Wilaya katika kata ya Kasuga na Kanyonza Jumanne 29 Julai, 2025 na kuambatana na Wataalam mbalimbali wa Serikali kuu na Halmashauri, amesisitiza Wananchi kujikita katika ulimaji wa zao la parachichi kisasa pamoja na michikichi.
Col.Mallasa ameeleza kuwa Wilaya imedhamiria kulima zao la parachichi kibiashara eneo la Mtendeli kata ya Kasanda ambapo zaidi ya hekari 1000 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha parachichi kupitia kilimo cha ‘block farming’ kinachosimamiwa na Wizara ya kilimo ambapo watajenga miundo mbinu, kugawa mbegu, kuleta matrekta, pembejeo na kusimamia kwa karibu ambapo Wananchi watagawiwa maeneo ndani ya kambi ya mtendeli ili kulima parachichi kwa faida na Halmashauri itaweza kupata kipato kupitia ushuru utakaotozwa hapo baadaye.
Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa TARI wataanzisha kituo cha utafiti wa mbegu katika Wilaya ya Kakonko na tayari wameomba eneo kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho na taratibu zinaendelea kuwawezesha kupata eneo hilo. Suala hilo litasidia wananchi kupata mbegu bora na utafiti utawezesha wakulima kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kilimo ikiwemo magonjwa.
Renatus Kagoroba, mkazi wa Kasuga,ameishukuru Serikali kwa kuleta kilimo cha parachichi kwani ni zao la kudumu hivyo ameomba Serikali kuongeza eneo karibu na eneo lililotengwa kwa ajili ya kilimo cha parachichi ili wananchi walio nje na kata ya Kasanda wapate maeneo kwa ajili ya kulima zao la parachichi pia.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ameeleza amelichukua hilo na tayari wameanza kulifanyia kazi ili kuwezesha Wananchi walio nje ya kata ya Kasanda kushiriki pia katika kilimo cha parachichi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa