Kakonko, 20 Mei 2025 – Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko limefanya kikao chake cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Fidel Chiza Nderego, aliyeeleza kuwa hali ya halmashauri ni nzuri na ushirikiano miongoni mwa viongozi umeimarika, hivyo akatoa wito wa kuendeleza mshikamano huo kwa maslahi ya wananchi.
Katika mkutano huo, wenyeviti wa kamati mbalimbali waliwasilisha taarifa na hoja mbalimbali zikiangazia utekelezaji wa shughuli za maendeleo, ustawi wa jamii na utawala bora.
Kamati ya kudhibiti UKIMWI ilijadili upatikanaji wa mipira ya kike ya kujikinga, ambapo Mwenyekiti aliahidi kuwa vifaa hivyo, vilivyoagizwa pamoja na vifaa vingine vya hospitali, vitapatikana ndani ya wiki moja.
Kamati ya Maadili ilitoa pongezi kwa madiwani wote kwa kutokuwa na malalamiko ya ukiukwaji wa maadili katika kipindi cha robo hii, hali inayoonesha nidhamu na uwajibikaji miongoni mwao.
Kamati ya Elimu, Afya na Maji ilitoa hoja ya kuongeza shule ya sekondari katika Kata ya Gwarama ili kupunguza umbali wa wanafunzi. Mkurugenzi Mtendaji, Ndaki Stephano Mhuli, alieleza kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa shule kila mwaka, na kwamba Gwarama iko kwenye mpango huo. Aliongeza kuwa shule ya Sekondari Muhange inapendekezwa kuwa shule ya upili (high school), na ujenzi wa shule mpya katika kijiji cha Mbizi pia upo kwenye mipango.
Kamati ya Huduma za Kiuchumi, Ujenzi na Mazingira iliwasilisha taarifa yake bila hoja yoyote kuibuliwa, huku kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ikijadili changamoto ya upatikanaji wa fedha za walengwa wa TASAF. Mkurugenzi Mtendaji alifafanua kuwa changamoto hiyo ilitokana na mabadiliko ya kimfumo katika ngazi ya kitaifa baina ya mifumo ya benki na serikali, lakini fedha hizo zitarudishwa kwa walengwa.
Afisa kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Uongozi, Patrick Shayo, aliwakumbusha viongozi wote wa umma kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni kila mwaka kabla ya tarehe 30 Desemba kupitia mfumo wa ODS, huku viongozi wanaomaliza muda wao wakitakiwa kuwasilisha tamko hilo ndani ya siku 90.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Kigoma, CPA Gwamaka Alfred Mtalila, alieleza kuhusu utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote na kuhimiza wananchi kujiunga na bima kupitia kitita cha jamii kwa Tsh 150,000 kwa mwaka. Alibainisha kuwa huduma hiyo inajumuisha huduma 277, huku TASAF ikitumika kuwaainisha wananchi wasio na uwezo ili kupata bima hiyo kwa msaada wa serikali.
Mwakilishi wa Meneja wa SIDO Kigoma, Mhandisi Alexander Nicholaus Mpuya, alieleza majukumu ya shirika hilo katika kusaidia viwanda vidogo, masoko, mikopo na ushauri wa kibiashara. Alieleza kuwa SIDO imesaidia ujenzi wa viwanda vidogo katika kata ya Gwarama, Kiga na Muhange. Alitoa wito kwa wananchi kushiriki mafunzo ya uendeshaji wa biashara.
Mkurugenzi Mtendaji, Ndaki Stephano Mhuli, alieleza mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo:
Ujenzi wa vibanda vya soko la Kakonko unaokamilika mwezi Mei 2025, na utazinduliwa rasmi tarehe 1 Juni 2025.
Ujenzi wa stendi mpya ya mabasi unaotarajiwa kukamilika na kukabidhiwa ifikapo tarehe 30 Juni 2025.
Kupokea watumishi wapya 40 katika kada mbalimbali.
Ziara ya mafunzo Wilayani Muleba kuhusu kilimo cha ‘block farming’ ambapo ekari 1,530 zimetengwa kwa ajili ya mazao kama parachichi, kwa vijana, wanawake na makundi mengine.
Kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Mei 2025, zaidi ya wananchi 4,851 waliandikishwa na jina la jimbo likabadilishwa kutoka Buyungu na sasa kuitwa Jimbo la Kakonko.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, pamoja na mwakilishi wa mkoa Bw. Moshi Hussein Muhini, waliipongeza Wilaya kwa usimamizi mzuri wa miradi na kuhimiza kukamilisha miradi yote ifikapo tarehe 15 Juni 2025, pamoja na kufanyia kazi hoja za CAG.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kakonko, Ndugu Saamoja Sadock Ndilaliha, alisifu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na ushirikiano wa kisiasa, akisisitiza kuwa siasa siyo uadui bali ni jukwaa la kushirikiana kwa maendeleo ya wananchi.
Katibu wa Baraza alitoa shukrani kwa viongozi wa idara, dini, siasa na madiwani kwa ushirikiano mzuri ambao umechangia ongezeko la mapato ya halmashauri kutoka chini ya bilioni moja hadi kufikia bilioni 1.88.
Akifunga kikao, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Fidel Chiza Nderego, aliwashukuru madiwani kwa uvumilivu na mchango wao katika maendeleo, na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa usimamizi mzuri wa miradi, huku akiahidi kuwa halmashauri itaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika maendeleo ya wananchi wa Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa