Baraza la madiwani Wilayani Kakonko limekataa kupokea miradi ya maji wa Vijiji 4 uliokuwa ukitekelezwa tangu mwaka 2012 na kumuondolea majukumu mkuu wa Idara ya maji kupisha uchunguzi katika kikao cha robo ya pili kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Akitoa maamuzi ya Baraza la madiwani, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye alikuwa akiendesha mkutano huo, Toyi Butono alieleza kuwa wamechukua hatua hiyo baada ya kuona miradi ya maji ya Vijiji 4 imekamilika lakini ina kasoro nyingi hivyo wananchi kushindwa kupata huduma ya maji.
“Madiwani wa Chama cha Mapinduzi pamoja na madiwani wa upinzani kwa pamoja tumekataa miradi ya maji ya Vijiji vinne vya Nyagwijima, Kiduduye, Katanga/Ilabiro na Muhange na tunamuondolea majukumu ya ukuu wa Idara Mhandisi wa Maji ili kupisha uchunguzi.” alisema makamu Mwenyekiti.
Mhandisi wa maji aliyeondolewa majukumu yake ya ukuu wa Idara ili kupisha uchunguzi ni injinia Elinathan Eliya Mkuu wa Idara ya maji aliyekuwa akisimamia miradi hiyo kwa kushirikiana na Wilaya ya Kibondo.
Skimu ya maji ya vijiji vya Muhange, Nyagwijima, Kiduduye, Katanga/Ilabiro na Kiga ni miradi iliyoingizwa katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kutekelezwa pamoja na miradi mingine ya Kibondo.
Ujenzi wa skimu ya maji kijiji cha Muhange ulianza Desemba 2012 na Mkandarasi aliyejenga mradi huu ni Famoyo Contractors kutoka Kasulu. Halmashauri ya Wilaya Kibondo ndiyo iliyosaini Mkataba wa Mradi huu na ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa Mradi akishirikiana na mhandisi wa Halmashauri ya Kakonko. Gharama za Mradi ni Tsh 820,591,309.90.
Aidha mradi wa Skimu ya maji ya kijiji cha Kiduduye ulianza mwaka 2013 na mkandarasi Karago Enterprises toka Dodoma.
Kwa upande wa mradi wa Skimu ya maji vijiji vya Katanga na Ilabiro ulianza mwaka 2013 na mkandarasi aliyesaini mkataba huu ni kampuni ya Y.N investment kutoka Dar es salam. Halmashauri ya Wilaya Kibondo ndiyo iliyoratibu shughuli za ushauri wa kitalaaam baada ya Mtalaam mshauri kusitishwa mkataba wake.
Mradi wa Skimu ya maji kijiji cha Nyagwijima ulianza desemba 2012 na Mkandarasi aliyejenga mradi huu ni Karago Enterprises kutoka Dodoma.
Miradi hiyo ilikuwa ikitekelezwa katika Vijiji 5 ambapo mradi wa maji wa Kijiji cha Kiga ndio pekee uliokubaliwa na Baraza la Madiwani kutokana kufanya kazi vizuri.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa