Benki ya CRDB tawi la Kakonko imeingia mkataba wa kufunga mfumo wa ‘’Hospital card Management system’’ (HCMS) na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, siku ya jana Julai 17,2023, katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Meneja wa benki ya CRDB Tawi la Kakonko Kesibe Mwalongo, Ameomba ushirikiano kutoka kwa Menejimenti wakati wa utekelezaji wa jukumu la kukusanya mapato kupitia mfumo wa HCMS ili kuongeza mapato.
Meneja Mwalongo ameeleza kuwa kwa kipindi kifupi walichofanya kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko tayari wamechangia Benchi 10 za wagonjwa katika hospitali ya Wilaya na Madawati 50 katika Shule ya Msingi Ruyenzi.
Yohana Bunzali, Meneja Uhusiano Biashara ya Serikali kanda ya Magharibi Ameeleza faida za kufunga mfumo wa ‘’Hospital card Management system’’ (HCMS) katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko kupitia mfumo huo itadhibiti upotevu wa mapato na kuongezeka kwa mapato. Benki ya CRDB inatoa huduma ya mikopo kwa watumishi ambapo mpaka sasa inatoa mkopo kiasi cha milioni mia mbili kwa riba nafuu sawa na asilimia 13% kama ukikopa kwa mwaka 1-2, kuna 15% kama ukikopa kwa miaka 2-5.
Vile vile kwa watumishi na wananchi wote ambao wana akaunti ya CRDB ikitokea amefariki Benki inatoa mkono wa pole milioni 2 na kama mke na mme katika familia walikua na akaunti ya CRDB Benki inatoa mkono wa pole milioni 4 na endapo walikuwa na mkopo wanapewa mkono wa pole milioni 1.
Aidha ameeleza kwa watumishi ambao wana kadi ya CRDB hawahitaji kufungua akaunti nyingine badala yake unatumia kadi ya ‘Hospital card business’ kulipia bili pia kwa watumishi wote ambao mishahara yao inapitia Benki ya CRDB kadi zao zitatumika kulipia bili za Hospitali.
Kidagaa Kubalunga, Meneja Uhusiano Biashara ya Mawakala na Huduma mbadala za Kibenki kanda ya Magharibi ameeleza kuwa Benki ya CRDB inatoa kadi za ‘credit card’ kwa watumishi ambao misharaha yao inapitia Benki ya CRDB na inaanzia laki 5 hadi Milioni 20 na kadi hiyo inakuwezesha kulipia huduma zote bila kuchangia chochote kwa muda wa siku 50 na riba yake unaruhusiwa kulipia kuanzia 20%.
Vile vile ameeleza Benki ya CRDB ina uzoefu wa kufunga mfumo wa Hospital card Management system (HCMS) kwa muda mrefu kwani toka mwaka 2002 Benki ndipo ilipoanza kufunga mfumo wa Hospital card Management system (HCMS) katika Hospitali pia imefunga mfumo huo katika Hospitali kubwa zenye wagonjwa wengi na mapato yao ni makubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Ndaki Stephano Mhuli amewahimiza watumishi kufungua akaunti za benki na kuangalia mahali ambapo huduma zinatolewa kwa ubora zaidi ili kupata matokeo kwa haraka.
Mkurugenzi Ndaki ameipongeza Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Halmashauri na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa