Wananchi wa Kata ya Kasanda wamehimizwa juu ya utunzaji wa mazingira na kusisitizwa kupanda miti itakayowasaidia kukua kiuchumi na kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kizazi cha sasa na cha baadae.
Akizungumza na wananchi siku ya Jumatatu Mei 22, 2023 wakati akitoa elimu ya utunzaji wa Mazingira katika Kata ya Kasanda Wilayani Kakonko, Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Dar es Saalam kwa kushirikiana na Shirika la REDESO, Michael David Rikanga amesema kuwa ukataji wa miti hovyo unaweza kusababisha ukame ambao unaweza kuwa chanzo cha wananchi kushuka kiuchumi hivyo waepuke kukata miti hovyo na badala yake waendelee kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira.
Shabani Hassan Mwakilishi wa Shirika la REDESO (Relief to Development Society) ameeleza kuwa wamekutana na Wananchi wa Kata ya Kasanda na kuwaelimisha kuhusu mazingira na kuibua changamoto ambazo zilisababishwa na wakimbizi waliokuwa wananishi katika kambi ya Mtendeli iliyopo Wilayani Kakonko.
Alexander Mwalemba Mtendaji wa Kata ya Kasanda ameeleza kuwa kama kata wamejipanga kufanya mikutano ya hadhara kuanzia ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Kata kwa ujumla ili jamii iwe na uelewa juu ya utunzaji wa mazingira.
Aidha kupitia elimu waliyopewa wataendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wapande miti na kuweka mikakati kwa wakulima pindi watakapokuwa wanaandaa mashamba kwa ajili ya kilimo kuhakikisha wanachukua barua kwenye Ofisi ya Kijiji ili kudhibiti ukataji wa miti hovyo na uchomaji wa misitu hivyo kusaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kata ya Kasanda.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasanda Thomas Gwamikiko amewashukuru wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu Dar es Saalam (UDSM) na Shirika la REDESO kwa kufika Kasanda kwa ajili ya kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira hivyo amewaomba wananchi kufuata kile walichoelekezwa kwani itawasaidia kutunza mazingira na kujiepusha kukata miti hovyo.
Kwa upande wake Kezia Uwezo, Mwakilishi wa Vijana ameahidi kuwaelimisha vijana wenzake umuhimu wa kupanda miti na madhara ya ukataji miti lengo ikiwa ni kutunza mazingira ili kuhakikisha Jamii inakuwa na Maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa