Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col.Evance Mallasa Jumamosi Januari 25, 2025 amefungua rasmi wiki ya sheria kwa kuongoza matembezi akiambatana na watumishi wa Serikali na wadau mbalimbali katika viwanja vya mahakama ya mwanzo.
Akizungumza wakati wa kufungua maadhimisho hayo, Col.Evance Mallasa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi ameiomba mahakama pamoja na Wadau wake kutumia muda huo kutoa elimu kwa umma juu ya jukumu zima la utoaji haki kwa wananchi, kutoa msaada wa kisheria, kusikiliza kero na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo mzima wa utoaji haki na utendaji wa shughuli za kimahakama.
Aidha ameeleza kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuwajengea uelewa wananchi wote juu ya uendeshaji wa mashauri mahakamani kwani suala la haki madai ni la jamii nzima hivyo kwa ujumla wanapaswa kufuatilia na kutambua wajibu walionao kulingana na kazi wanazozifanya wakati huohuo jambo hilo litawasaidia wananchi kutambua haki zao za kisheria na taratibu za kimahakama.
Vilevile mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa kupitia kauli mbiu isemayo “Tanzania ya 2050 nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya Taifa ya Maendeleo’’. Hivyo kupitia kauli hiyo dira ya 2050 imejikita katika kuhimiza ukuaji wa kipato cha mtanzania kuwa na uchumi wa kati.
Mgeni rasmi ameongeza kuwa ili lengo liweze kufikiwa, Mahakama na Taasisi zinazohusika na utatuzi wa madai zina jukumu la kufanya kazi kwa weledi na kasi kubwa ili kuhakikisha kila mtanzania anafikia malengo kwa kukuza uchumi wake na nchi kwa ujumla.
Hatahivyo amewataka wananchi kuendelea kutatua changamoto zao kisheria na kujiepusha na uvunjifu wa sheria kwa kujichukulia sheria mkononi kwani jambo hilo linaweza kusababisha uvunjifu amani hivyo amesisitiza wananchi kuendelea kufuata sheria za nchi.
“Kila mwananchi analo jukumu la kujali haki zake na watu wengine hata hivyo kumekuwa na wananchi wanaojichukulia sheria mkononi, jambo hilo ni kinyume na sheria”, alieleza Col.Mallasa.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mhe.Ambilike Kyamba, amesema wiki ya Sheria ni kiashiria cha kuanza shughuli za kisheria kwa mwaka mpya 2025 hivyo wiki hii ya kisheria inatoa fursa kwa wananchi kufika kujifunza majukumu ya mahakama na kupata elimu na ushauri wa kisheria kupitia kwa wadau wanaotoa huduma mbalimbali za kisheria hadi kilele cha siku ya sheria Februari 03, 2025 hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo yote ambayo watakuwa wakitoa elimu ya kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa