Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imepokea kiasi cha fedha za kitanzania Millioni Mia Saba na Sitini (Tsh. 760,000,000/=) kutoka Serikali kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa madhumuni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa thelathini na nane (38) ikiwa ni Maandalizi na Mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha Kwanza kwa Mwaka 2023.
Mkuu wa wilaya ya kakonko kanali Evance Mallasa leo Jumatano Oktoba 12,2022 amefanya kikao na viongozi pamoja na wasimamizi wa miradi ya elimu kwa lengo la kuweka mikakati namna ya utekelezaji wa ujenzi wa madarasa hayo kwa viwango Bora.
Mkuu wa Wilaya ameitaka halmashauri kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji, wakuu wa shule na watendaji wa kata kuhakikisha wanazingatia kuchagua mafundi weledi watakaoomba kazi hizo za ujenzi na kuepukana na mafundi wasio kuwa waadilifu, Pia aliwaagiza maafisa manunuzi kuhakikisha mipango ya utekelezaji wa manunuzi ya vifaa vya ujenzi mapema, vile vile aliwaeleza wahandisi wa ujenzi wahakikishe wanakua maeneo ya ujenzi wakiwa na vitendea kazi vyao.
Aidha amewataka waheshimiwa madiwani, Maafisa tarafa, Watendaji wa kata na Watendaji wa vijiji kuwaeleza wananchi kuhusu fedha zilizotolewa na Mhe.Rais na kutambulisha miradi hiyo kwa kufanya mikutano ya hadhara ili kuwa na uelewa juu ya miradi itakayotekelezwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ndugu Ndaki Mhuli alimshukuru mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali Wilaya ya Kakonko, alieleza mara baada ya kupokea fedha hizo tayari taratibu za ujenzi zimeshaanza na alimhakikishia Mkuu wa wilaya kutimiza kazi ya ujenzi wa madarasa kwa wakati, hivyo aliomba ushirikiano wa kutosha kwa kamati mbali mbali za ujenzi, watendaji wote pamoja na wananchi kuwa waaminifu ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ndugu Fideli Nderego ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuleta fedha za maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya kakonko kwa lengo la kuboresha miundombinu na kukuza taaluma mashuleni.
Kikao hicho kimehudhuriwa na kamati ya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara na vitengo, Watendaji wa Kata na Vijiji, Waratibu Elimu Kata Na Wakuu wa Shule.
Mkuu wa Wilaya kanali Evance Mallasa ametoa maelekezo ya ujenzi wa madarasa 38 kukamilikia kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2022 hadi kufikia tarehe 1 Desemba, 2022.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa