Jumuiya ya Kolping Tanzania na Malteser International kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa vifaa tiba na madawa yenye thamani ya Tsh.88,295,430 Wilayani Kakonko kwa ajili ya hospitali ya Wilaya pamoja na kituo cha upasuaji Mtendeli.
Msaada huo wa fedha umekabidhiwa na Muasisi na Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kolping Tanzania Fr.David Kamugisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Kakonko katika kituo cha Afya Mganza hivi karibuni.
Akikabidhi msaada huo wa Vifaa tiba na madawa Mkurugenzi wa Kolping Tanzania ameeleza kuwa msaada huo umegawanyika katika sehemu mbili ambapo vifaa tiba na madawa yenye thamani ya Tsh.Tsh.43,656,430 ni kwa ajili ya hospitali ya Wilaya ya Kakonko ambapo kwa sasa kituo cha Afya Mganza kinatumika kama hospitali ya Wilaya kikitoa huduma hadi maeneo ya jirani ya Wilaya ya Kakonko.
Aidha vifaa tiba na madawa yenye thamani ya Tsh.33,419,600 pamoja na ‘Power Inverter’ yenye thamani ya Tsh.10,620,000 vimetolewa kwa ajili ya kituo cha upasuaji Mtendeli.
Kituo cha upasuaji Mtendeli kipo katika kambi ya wakimbizi Mtendeli inayohudumia wakimbizi kutoka nchi ya Burundi na Wenyeji wa kambi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col. Hosea Ndagala ameshukuru kwa msaada wavifaa hivyo na kueleza vifaa hivyo vitaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na uwezo wa hospitali kuhudumia watu wengi zaidi na kuahidi kusimamia kikamilifu vifaa hivyo.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Masumbuko Stephano baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya vifaa hivyo ameahidi kuhakikisha vifaa hivyo vinaleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Msaada huo ni matokeo ya Juhudi za pamoja kati ya Malteser International na Jumuiya ya Kolping Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kuisaidia Serikali ya Tanzania kupunguza adha na makali kwa wakimbizi na wenyeji walio karibu na kambi za wakimbizi nchini Tanzania hususan Wilayani Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa