Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mhe. Fidel Chiza Nderego amewahimiza Washiriki wa Mafunzo ya MEMKWA kuhakikisha wanazungumzia Ajenda ya Programu ya Elimisha Mtoto katika vikao na mikutano ya hadhara ya Kata na Vijiji ili kuzidi kuijengea jamiii uelewa na kushiriki katika ukarabati wa miundombinu iliyochakaa.
Mratibu wa MEMKWA Ndugu Majaliwa Tryphone, Afisa Elimu Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi wakati akiwasilisha taarifa alieleza lengo la Shirika la UNICEF kupitia programu ya Elimisha Mtoto ni kuhakikisha wanajenga miundombinu ya muda na kukarabati Madarasa na Vyoo kwa ajili ya watoto ambao wako nje ya mfumo rasmi wa Elimu ili waweze kujifunza katika mazingira safi na salama .
“Washiriki wa Mafunzo wanao wajibu wa kwenda kuwaelimisha wazazi/walezi na kuwashirikisha wadau wa Elimu ili wajenge miundombinu ya madarasa na Vyoo pamoja na vitakasa mikono kwa kuwa Shirika la UNICEF haliwezi kujenga miundombinu hiyo bali wao wanachangia katika ukarabati na ukamilishaji majengo hayo ambayo yamechakaa au yamejengwa na nguvu za wananchi na hayakukamilika”, alieleza mratibu Majaliwa.
Mafunzo ya uhamasishaji wa jamii juu ya ukarabati wa miundombinu ya madarasa ya MEMKWA yaani Mpango wa Elimu kwa Watoto walioikosa yalifanyikwa mwishoni mwa wiki Machi 17, 2023 katika Ukumbi mdogo uliopo Ofisi za Halmashauri eneo la Kanyamfisi.
Mafunzo hayo ambayo yanafadhiliwa na Shirika la UNICEF kupitia Programu ya Elimisha Mtoto yamewahusisha Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vya Gwarama, Kanyonza, Mugunzu, Katanga na Nyamtukuza.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa