Wajumbe wa kamati ya Ushauri ya Wilaya wameridhia mapendekezo ya kubadilisha jina la Jimbo la Buyungu kuitwa jimbo la Kakonko ili kufanana na jina la Wilaya na Halmashauri.
Mapendekezo hayo yamepitishwa katika kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya kilichoongozwa na mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Kamati ya Usalama, Wakuu wa taasisi, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri, Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa kata, Viongozi wa dini, Viongozi wa Vyama vya siasa na kufanyika leo Alhamisi Machi 13, 2025 katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
"Jina Buyungu ni zuri lina utambulisho wa kiasili ila Wilaya ya Kakonko ina watu wenye asili tofauti tofauti hivyo linaleta utengano lakini jina la Kakonko linaunganisha jamii yote", alieleza Col.Mallasa .
Kaimu Mkurugenzi mtendaji Michael Magesa amefafanua kuwa Wilaya inaonyesha mgawanyo wa madaraka, halmashauri inawakilisha utoaji wa huduma na jimbo lina maana ya uwakilishi wa wananchi hivyo lengo la Serikalini ni kuhusianisha jina la jimbo, Wilaya na Halmashauri kuwa moja ili kuwa rahisi kutambulika na kufikiwq na fursa nyingi zaidi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wameeleza kubadilisha jina la Buyungu kuwa Kakonko haimaanishi kupoteza asili ya jina Buyungu linalowakilisha desturi za Wayungu bali lengo ni kuwa na jina linalowakilisha dira na dhima ya wanajamii wote wanaoishi Kakonko.
Aidha wameeleza kuwa lengo ni kuwa na utambulisho mmoja hususani bungeni na Serikalini kwani watu wengi walipokuwa wakitajiwa jimbo la Buyungu ilikuwa ni vigumu kujua jimbo hilo lipo wapi kijeografia.
Wilaya ya Kakonko ilianzishwa rasmi mwaka 2011 na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ilianza rasmi mwaka 2013.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa