Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko jana tarehe 10 Juni, 2024 imetembelea na kukagua ujenzi wa Jengo la upasuaji, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti pamoja na njia za watembea kwa miguu unaoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi unaoendelea Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya, Dr.Fredrick Mshana ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni mia nane (800,000,000/=) kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa majengo mawili na njia za watembea kwa miguu katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko lengo ikiwa kuwasogezea wananchi huduma bora pamoja na watoa huduma kutoa huduma katika mazingira yaliyo bora.
Akieleza hatua iliyofikiwa, Mganga mfawidhi ameeleza kuwa ujenzi umefikia hatua nzuri ambapo jengo la upasuaji limefikia hatua ya kupiga plasta na kuweka mbao kwa ajili ya kupigilia ‘ceiling board’ pamoja na mfumo wa umeme.
Dr.Mshana ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti (mochwari) upo katika hatua ya kupandisha boma wakati ujenzi wa njia za watembea kwa miguu (walk ways) upo katika hatua ya umaliziaji ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika katika ujenzi wa majengo mawili ambayo ni jengo la upasuaji na mochwari ni Milioni mia nne tisini na tatu kumi na tisa elfu mia mbili sabini na tano na senti themanini na nane (Tsh.493,019,275.88).
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mhe.Fidel Chiza Nderego ameeleza kuwa kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi na kuwapongeza wasimamizi wa mradi huo.
Hata hivyo Mhe.Nderego amewataka watumishi kutimiza wajibu wao kwa asilimia 100 mahala pa kazi na kuwataka pale wanapokutana na changamoto waweze kutoa taarifa kwa Viongozi wao ili changamoto hizo ziweze kushughulikiwa.
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetembelea miradi mitatu ukiwemo Undelezaji wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ambapo kwa sasa kuna ujenzi wa Ukumbi wa Halmashauri, fensi, kibanda cha mlinzi na uwekaji wa mifumo ya Mawasiliano kwa gharama ya Tshs.1,000,000,000, Ujenzi wa nyumba 08 za wakuu wa Idara kwa gharama ya Tshs.640,000,000, Ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji kwa gharama ya Tshs.180,000,000 na ujenzi wa jengo la upasuaji njia ya waenda kwa miguu na mochwari katika hospitali ya Wilaya kwa gharama ya Tshs.800,000,000.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Fidel Chiza Nderego aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji, Ndaki Stephano Mhuli, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Abdallah Magembe, Wajumbe wa kamati ya fedha, Mwakilishi wa Katibu Tawala wilaya, Maafisa Tarafa na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa