Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) Col.Evance Mallasa ameongoza kikao cha kupitia rasimu na bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko yenye jumla ya Tshs.26,831,284,119 pamoja na bajeti za taasisi za Serikali Kuu ikiwemo TARURA na RUWASA zenye zaidi ya bilioni 4, siku ya Jumanne, Februari 11, 2025.
Akifungua kikao, Mwenyekiti wa kamati ameeleza kuwa ni vyema Kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa majukumu ili kuleta matokeo yenye tija.
Afisa Mipango wa Halmashauri, Michael Faraay amewasilisha bajeti ya halmashauri kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji yenye Jumla ya Tshs.26,831,284,119 ikiwa na vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuajiri watumishi wapya 174 na kupandisha vyeo watumishi 526.
Kwa upande wa taasisi za Serikali, Meneja wa Tarura Eng.John Ambrose ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini TARURA inaomba kuidhinishiwa kiasi cha bilioni 2.27 kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa Barabara zenye urefu wa kilomita 136.54 kupitia mfuko wa Barabara, mfuko wa Jimbo na mfuko wa tozo ya mafuta.
Meneja TARURA Ameongeza kuwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo wameomba milioni 500 ili kufungua Barabara ya Nyakavyiru Kwenda Kijiji cha Luhuru yenye urefu wa kilomita 44 na kupitia mfuko wa tozo ya mafuta wamelenga kutengeneza barabra za kuingia na kutoka stendi yam abasi zenye urefu wa mita 300, milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara inayoelekea makao makuu ya Halmashauri na milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Itumbiko na uwekaji wa taa za barabarani.
Kaimu Meneja wa RUWASA, Martha Mwasimba alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira wanategemea kutekeleza miradi mbalimbali inayogharimu zaidi ya bilioni 1.9 ikiwemo ukamilishaji ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Luhuru kwa milioni 510, Kabare kwa milioni 663, upanuzi na ukarabati wa maji Kijiji cha Bukirilo Milioni 370, ujenzi wa Miundo mbinu ya kutibu maji ili kuondoa tope katika Kijiji cha Muhange na Kabare kwa gharama ya milioni 140 na upanuzi wa ukarabati wa skimu za maji Kijiji cha Gwarama, Churazo, Kinyinya, Nyanzige, Kasongati na Nyabibuye kwa gharama ya milioni 310.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa