Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa amewahimiza Waheshimiwa Madiwani na Halmashauri kuangalia namna ya kuwasaidia Wanafunzi wa shule za Sekondari wanaotembea umbali mrefu ikiwemo kujenga mabweni na vibweta vya kujisomea nyakati za Mitihani ili kupunguza adha ya wanafunzi ambao hawafiki Shuleni kutokana na kutembea umbali mrefu.
Amesema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi Februari, 2023, katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Col.Mallasa alieleza kuna umuhimu wa kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabweni Wanafunzi kwani wanapata changamoto ya kutembea umbali mrefu wakati huo hali ya hewa si rafiki na mvua zinaendelea kunyesha hivyo kujikuta hawawezi kuhudhuria siku zote za masomo yao.
Aidha alihimiza kuwa kila Shule inatakiwa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi angalau mlo mmoja kwa siku, hivyo Wazazi/Walezi wanao wajibu wa kuchangia chakula Shuleni ili Watoto wapate huduma ya chakula na kusisitiza kila Shule iwe na shamba darasa kwa ajili ya kulima mazao ya Chakula na kila mwanafunzi apande angalau mti mmoja wa matunda ili Watoto wawe na afya bora.
Aliongeza kuwa jamii bado ina mwamko duni juu ya umuhimu wa Elimu kwani mpaka sasa katika zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza Wilaya ya Kakonko bado haijafikisha asilimia 100% hivyo Watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Elimu Kata pamoja na Walimu wakuu wa Shule wahakikishe Watoto wote ambao wamefikia umri wa kuanza Shule waandikishwe na uhamasishaji juu ya umuhimu wa Elimu uendelee kufanyika kwa wananchi.
“Sisi Viongozi tumepata fursa ya kuweza kuelewa umuhimu wa Elimu tutumie nafasi hii kuweza kuwaelimisha na wenzetu”, alihitimisha Mkuu wa Wilaya Col.Mallasa.
Wilaya ya Kakonko ina jumla ya shule za Sekondari 15 ambapo kati ya hizo shule 11 zina hosteli na shule 4 hazina hosteli.
Aidha kwa sasa uandikishaji kwa elimu ya awali na Msingi umefikia 100% na Sekondari 99.5%.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa