Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Aggrey John Magwaza ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo ameyahimiza Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa huduma kwa kuzingatia misingi na maadili ya kitanzania.
Kanali Magwaza amesema hayo katika Warsha ya Mkutano wadau wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Wilayani Kakonko iliyofanyika Mei 16, 2023, katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Mkuu wa Wilaya ameeleza katika kipindi hiki yameibuka mashirika yanayounga mkono suala la ndoa za jinsia moja jambo ambalo si jema katika jamii za kiafrika, hivyo ameyasisitiza mashirika kutotekeleza shughuli hizo hata kama ni sehemu ya majukumu yao.
Aidha katika hotuba yake ameeleza anatambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na anayapongeza kwa mchango huo vile vile kuna baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali hapa nchini yamekuwa hayazingatii wajibu wao wa kisheria hivyo kusababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wadau wa maendeleo wanaotoa fedha zao kuchangia katika juhudi za nchi kujiletea maendeleo.
‘Naiagiza Halmashauri kupitia ofisi ya maendeleo ya jamii kuhakikisha mashirika yote yasiyokuwa ya kiserikali yanatekeleza shughuli zao kulingana na usajili, malengo na vipaumbele vya taifa, aidha ninayataka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yajielekeze kufanya kazi maeneo yenye uhitaji ikiwemo vijiji badala ya kujikita maeneo ya mjini pekee’. Alisema kanali Aggrey Magwaza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndaki Stephano Mhuli ameeleza mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekuwa na msaada mkubwa sana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwani mashirika yanafanya kazi nzuri ya kuchangia katika ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa wodi ya mama na mtoto pia wamefanya shughuli ya ugawaji wa taulo kwa watoto wa kike shuleni na ugawaji wa baiskeli kwa wanafunzi wa kike wanaotembea umbali mrefu hasa wanaoishi katika mazingira magumu.
‘Kwa hiyo tuwapongeze Mashirika mmekuwa wadau wakubwa sana wa maendeleo katika Wilaya ya Kakonko na sisi tuseme tumefurahi kuwa na nyie’, Alisema Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Jamii (W) Mustapha Mtungwe ameeleza kuna baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekuwa yakiunga mkono tabia zisizofaa na zisizokubalika kwa mujibu wa maadili ya kitanzania hivyo kanuni zinatoa onyo kwa mashirika kutoshiriki na kutoingia mikataba ambayo inashusha hadhi ama Uhuru wa Taifa.
Bonita Mpokwa kutoka Shirika la ‘Plan international’ ambaye ni Mratibu wa mradi wa KAGIS (Keeping Adolescent Girls in School) katika Wilaya ya Kakonko na Kibondo ameeleza kuwa amefurahi sana kushiriki katika kikao kwa sababu kama mdau wa umoja wa mashirika yasiyo ya kiserikali wameweza kukutanishwa na wadau wengine wa mashirika na wamezungumza vitu mbalimbali ambavyo vinahusiana na utekelezaji wa miradi ambayo wanaifanya katika Wilaya ya Kakonko.
‘Sisi tukiwa kama wadau wa maendeleo ya Jamii kwa upande wa miradi ambayo tunaitekeleza tumeweza kushiriki na kuangalia wengine wanafanya nini na sisi tunafanya nini na wapi tunaweza kukutana na wapi tunaweza kutatua changamoto kwa pamoja kwahiyo kimekuwa ni kikao cha tija ambacho kinatuonyesha nani anafanya nini na wewe unafanya nini na wapi tunaweza kuingiliana, kwa hiyo mimi nimefurahi sana na ninashukuru nimeweza kushiriki kwa niaba ya timu ya KAGIS’, Amesema Bonita.
Dr. Julius Zelote meneja wa THPS Mkoa wa Kigoma ameeleza kuna umuhimu mkubwa sana wa mashirika yasiyo ya kiserikali kukutana pamoja na ameipongeza Wilaya ya Kakonko kwa kuwalika katika kikao hicho ambazo ni mara ya kwanza lakini kinawakutanisha wadau mbalimbali ambao wanachangia maendeleo, pia kikao hiki kinasaidia kujua wenzako wanafanya nini na inasaidia wakati wa kuandaa mpango kazi kuepuka kupeleka miradi katika eneo moja tu wakati mahitaji ni mengi hivyo ni kitu kizuri kufahamu mwenzako anafanya nini na wewe unaweza kuchangia nini kwenye maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa