Mheshimiwa Aloyce John Kamamba Mbunge wa Jimbo la Buyungu kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo la Buyungu amechangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya Tshs. 5,000,000/= (Milioni Tano) kwa ajili ya ukarabati wa vyumba (5) vitano vya Madarasa katika Shule ya Sekondari Kashoza.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge mwanzoni mwa mwezi Mei, 2023, Bwana Eliud Jackson ambaye ni katibu wa Mbunge ameeleza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mfuko wa jimbo umechangia Mifuko 100 ya Saruji katika Shule ya Sekondari Kashoza kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya madarasa ambayo imechakaa ili kuboresha mazingira salama ya kujifunzia kwa Wanafunzi.
Aidha Mhe. Kamamba ameagiza uongozi wa Shule kwa kushirikiana na Mhe. Diwani wa kata ya Nyabibuye, Afisa Elimu Kata, Mtendaji wa kata na kijiji pamoja na Wananchi kuhakikisha wanasimamia rasilimali zote ili zitumike kama zilivyopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Kashoza, Shukran Selege Nyaminya alieleza amefurahishwa na kitendo ambacho amekifanya Mhe. Mbunge kupitia mfuko wa Jimbo na anamshukuru kwa jitihada hizo kwa kuchangia saruji mifuko 100 ambazo zitasaidia kukarabati madarasa matano yaliyochakaa, pia anaahidi madarasa hayo yataanza kutumiwa na wanafunzi pindi yatakapokamilika kukarabatiwa.
Naye Ndugu Samwel Alfred, Afisa Elimu Kata Nyabibuye alieleza katika kata ya Nyabibuye hali ya miundombinu iko vizuri lakini baadhi ya Shule zina changamoto ya miundombinu chakavu moja wapo ikiwa ni Shule ya Sekondari Kashoza hivyo kupitia mfuko wa jimbo la Buyungu ambao Mwenyekiti wake ni Mhe. Aloyce Kamamba anamshukuru kwa mchango wake kwani wanafunzi watakuwa wanajifunza katika mazingira salama na kuahidi kusimamia mradi huo kwa ufanisi ili kufikia malengo.
Edison Kilishahu, Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Kashoza amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Buyungu kwa kupeleka mifuko ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa madarasa kwani walikuwa wakibanana madarasani hivyo uboreshwaji wa miundombinu hiyo utawasaidia kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia na wameahidi kuitunza miundombinu hiyo.
Wajumbe wa mfuko wa jimbo wamekabidhi vifaa mbalimbali katika Kata ya Nyamtukuza, Nyabibuye na Gwarama vyenye thamani ya Tshs. 77,136,000/= kukamilisha miradi iliyofadhiliwa na mfuko wa jimbo la Buyungu.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa