Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Mhe.Aloyce Kamamba, leo Jumatatu Machi 03, 2025 amekutana na kufanya kikao na Watumishi wa Halmashauri wa makao makuu huku akiwasisitiza kutumia rasiliamali na fedha zinatolewa na Serikali vizuri, kujiendeleza kielimu, kuwekeza na kujiandaa kustaafu.
Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri wanaofanya kazi katika ofisi za Halmashauri eneo la Kanyamfisi, Mhe.Kamamba amewasisitiza Watumishi kila mmoja kwa eneo lake kusimamia vizuri rasilimali na fedha zinazotolewa na Serikali ili kuleta manufaa katika jamii na vizazi vijavyo.
“Tuwe waaminifu kwenye kazi tunazopewa ili zitusaidie kupanda hatua inayofuata katika kazi zetu”, alieleza Mbunge wa Jimbo la Buyungu.
Aidha Mbunge ameongeza kuwa pamoja na kazi wanazofanya za kutumikia Wananchi, Watumishi wanapaswa kuanza kuwekeza kwa kujikita katika shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo na biashara kwa ajili ya maisha ya baadaye na kujiandaa kustaafu.
Mhe.Mbunge amefafanua kuwa kutunza fedha siyo jambo rahisi badala yake ni vizuri kuwekeza fedha kwa kujikita katika shughuli za ujasiriamali na miradi mara baada ya masaa ya kazi.
Vilevile, Mhe.Kamamba amewahimiza Watumishi wajiendeleze kieleimu na kitaaluma kwani elimu inaongeza thamani ya mtu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Michael Faraay amempongeza Mhe.Mbunge wa Jimbo la Buyungu kwa nasaa nzuri alizotoa kwa Watumishi na kuahidi kufanyia kazi yale aliyoyaeleza kwa manufaa ya Watumishi na jamii kwa ujumla.
Mhe.Fidel Chiza Nderego, Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye ameshiriki kikao hicho ameeleza watatoa ushirikiano wa dhati kwa jitihada anazofanya mheshimiwa mbunge kuleta maendeleo kwa Jimbo la Buyungu na Wananchi kwa ujumla.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Watumishi wameleza kufurahishwa na hatua ya Mheshimiwa Mbunge kuandaa kikao na kuzungumza na Watumishi huku akiwaasa kujikita katika uwekezaji na kujiandaa kustaafu kwani mambo hayo yataleta tija kwa Watumishi wote watakapozingatia na kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu, anafanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Jimbo akifanya mikutano na Wananchi, kugawa mashine za kudurufu kwenye ofisi za kata 13 ambapo zitatumika pia katika shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya kata.
Ziara hiyo imeanza tarehe 28.02.2025 na itamalizika tarehe 09.03.2025 ikihusisha Wataalam mbalimbali wa Halmashauri ambao wanatoa ufafanuzi kwa Wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa