Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imekabidhi rasmi mradi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 katika shule ya sayansi ya wasichana Kakonko iliyopo kata ya Kanyonza Wilayani Kakonko.
Akikabidhi bweni hilo lenye thamani ya Tsh.142,934,332 kwa Uongozi wa Halmashauri na shule, Paul Kawawa, Afisa Miradi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ameeleza kuwa bweni hilo limejengwa kwa viwango ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kuchochea maendeleo ya elimu kwa wasichana.
“Nawaomba walimu, wanafunzi pamoja na jamii nzima kwa ujumla kuhakikisha bweni hili linatunzwa kwa manufaa ya wanafunzi wa sasa na wa baadae”, Alisisitiza Bwana Kawawa.
Aidha ameendelea kusema kuwa ujenzi huo ni juhudi za Serikali kwa kushirikiana na mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuendelea kuboresha miundo mbinu ya elimu na kuhakikisha wanapata mazingira salama na rafiki ya kujifunza.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule ya Wasichana Kakonko, Alex Kagoma, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hasan, kwa kuendelea kuweka mipango madhubuti kuhakikisha wasichana wanapata elimu ipasavyo.
Aidha ameongeza kuwa Serikali imeitendea haki Wilaya ya Kakonko kwa kujenga miundo mbinu ya kielimu na kupunguza changamoto ya wanafunzi wengi kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutembea umbali mrefu.
Naye Elumva Juma, Mwanafunzi wa kidato cha Tatu,Shule ya wasichana Kakonko, ameishukuru mamlaka ya elimu Tanzania (TEA) kwa kufanikisha ujenzi wa bweni litakalowasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa kike hivyo kuahidi kulitunza bweni hilo kwa ajili ya kizazi kijacho.
Mhe.Alfred Elias, Diwani wa Kata ya Kanyonza ameeleza kuwa miaka ya nyuma wazazi walikuwa wakihangaika kupeleka wanafunzi shule zilizopo nje ya Halmashauri lakini baada ya Serikali kujenga shule hiyo na bweni kwa sasa wanafunzi wanapata elimu katika mazingira rafiki hivyo wanategemea miaka ijayo watapata wasomi wengi hususani wa sayansi na kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa