Mikataba 3 ya Miradi ya maji yenye thamani ya bilioni 1,573,000,000 imesainiwa na kupangwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 6 Wilayani Kakonko.
Kaimu mhandisi wa maji, Matwiga Victor Tandali ameeleza hayo katika hafla ya kusaini mikataba hiyo iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ambapo wakandarasi watatu wamesaini mikataba.
Mradi wa kwanza utakuwa ni ujenzi wa mradi wa maji Kakonko utakaogharimu milioni 299.6 na kutekelezwa na kampuni ya Santiago. Mradi huo unatokana na fedha za matokeo ya haraka (Quickwins) ambapo mradi utajikita katika kuchimba visima na kupanua mtandao na kufikisha maji makao makuu ya Halmashauri na maeneo ya jamii.
Bwana Matwiga ameongeza kuwa mradi wa pili utahusika katika kuweka nishati ya jua katika kata ya Gwanumpu na kugharimu milioni 623.2 na kutekelezwa na kampuni ya MS Gross.
Aidha mradi wa tatu utafanyika katika kata ya Nyabibuye ukilenga kufanya ukarabati mkubwa na kupanua maeneo ya huduma ya mradi ambao ni wa kutega unaogharimu milioni 660.2 na kutekelezwa na kampuni ya OBD.
Mhandisi wa maji ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya sekta ya maji kimkakati kwa kuangalia dira ya mwaka 2025 na ilani ya uchaguzi.
Diwani wa kata ya Nyabibuye ambaye ni mnufaika wa mradi, Stephen Munigankiko ameeleza kuwa wakazi wa Kijiji cha Nyabibuye walikuwa hawapati huduma ya maji hivyo mradi ukikamilika utakuwa ni msaada na mkombozi mkubwa kwao.
Mmoja wa mkandarasi aliyepata kazi, Santiago ameeleza kuwa wapo tayari kufanya kazi kwa moyo wanachohitaji ni kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi. Hata hivyo aliwaomba wanasiasa kufanya kazi zao za kisiasa na kutoa nafasi kwa wakandarasi kufanya kazi zao za kitaalam.
Kwa mujibu wa mhandisi Matwiga kwa sasa miradi ya maji inayotekelezwa Kakonko mjini imefikia hatua 45% lakini miradi itakapokamiika itafikia asilimia 65% wakati kwa upande wa vijijini ni 50% kwa sasa na inategemewa kufikia 58% miradi itakapokamilika.
Wadau wa maendeleo wakiwemo Water Mission wamefadhili mradi wa maji wa Kakonko mjini kwa kuchimba visima nakuweka nishati ya jua mabapo mradi umegharimu milioni 222.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa