Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa amewahimiza Wananchi wa Wilaya ya Kakonko kuwawekea hereni mifugo kabla ya tarehe 31 Oktoba, 2022 ambayo ndio mwisho wa zoezi hilo.
Col.Mallasa amefafanua umuhimu wa kuwawekea hereni mifugo wakati aikiendesha kikao cha tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri siku ya Alhamisi tarehe 20 Oktoba, 2022, kuwa itasaidia taarifa za mifugo kuingizwa katika mfumo wa kisasa wa kielektroniki ambapo popote mifugo itakapokwenda itatambulika na taarifa zake kujulikana.
Aidha Mkuu wa Wilaya aliendelea kueleza kuwa wawekezaji kutoka nje wanapofika kununua nyama wataweza kutambua iwapo mifugo imechanjwa na haina magonjwa hivyo kuongeza ununuzi wa mifugo hiyo.
Vilevile Col.Evance Mallasa alitoa wito kwa maafisa ugani kuwaelimisha Wananchi waliopo maeneo ya mipakani ili wajue kuwa mifugo inapowekewa hereni inatambulika kuwa ni ya Tanzania hata kama itavuka au kutoka nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dr.Godfrey Kayombo alieleza kuwa bei ya kuweka hereni kwa mifugo ni Tshs.1750 na iwapo Mwananchi hataweka hereni kwenye mifugo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini.
Kikao cha tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 kimehudhuriwa na Viongozi wa Chama Tawala (CCM) ngazi ya Wilaya, Wajumbe wa kamati ya Usalama, Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa dini, Wakuu wa Taasisi za Serikali, Wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Halmashauri, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa shule, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa