Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col. Evance Mallasa, amewataka wafanyabiashara Wilayani Kakonko kuwekeza katika sekta ya biashara na kujikita katika kilimo cha mazao ili kuhakikisha Wilaya ya Kakonko inapiga hatua katika Sekta ya biashara na uwekezaji kwani maeneo ya uwekezaji ni mengi.
Akizungumza na wajumbe wa baraza la biashara katika kikao kilichofanyika Ijumaa Oktoba 06, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ameeleza kuwa kikao cha baraza la biashara kinalenga kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoleta maendeleo na kutatua changamoto za wafanyabiashara.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Afisa Kilimo Dr.Godfrey Kayombo, aliwasilisha fursa za uwekezaji katika maeneo mbali mbali ya kilimo na mifugo na kueleza kuwa Halmashauri imetenga kiasi cha fedha 3,000,000/= kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kununua mbegu bora za mpunga kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuchochea biashara na uchumi katika Wilaya ya Kakonko.
Ameendelea kusema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa Kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo na mifugo inaendelea kuendesha mafunzo kwa wakulima kwa njia ya mashamba darasa ambapo kwa mwka huu wa fedha 2023/2024 wanategemea kuwa na mashamba darasa 57 ya kilimo cha Mahindi, Alizeti, Maharage, viazi lishe, Muhogo na Karanga kwa kata zote ndani ya Wilaya ya Kakonko pamoja na mashamba darasa 24 ya ufugaji wa kuku katika kata ya Katanga, Kasanda, Nyabibuye na Nyamtukuza.
Wafanyabiashara wamemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kakonko kuendelea kuwashirikisha katika Baraza la biashara na wameomba kuendeleza ushirikiano katika sekta binafsi na sekta ya umma na kuwaomba wataalamu kuwa karibu na wakulima kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu na kuwasogezea pembejeo za kilimo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndg. Michael Faaray, amewaomba wafanyabiashara kuhudhuria vikao vya ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Kata ili kutoa changamoto zao kwa lengo la kufikisha katika ngazi ya Halmashauri kwani Halmashauri imejipanga kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi ndani ya Wilaya ya Kakonko.
Baraza la biashara la Wilaya ya Kakonko limewakutanisha Viongozi wa Serikali Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wadau wa biashara ambao ni wafanya biashara wa Wilaya ya Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa