Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa ametoa wito kwa mahakama ya Wilaya ya Kakonko kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya taratibu za kuzingatia na kufuata ili waweze kutatua migogoro yao ya mashauri ya ndoa, talaka, ardhi, mirathi na kutambua taratibu za dhamana.
Amesema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Sheria yaliyofanyika katika majengo mapya ya Mahakama ya Wilaya ya Kakonko eneo la Kanyamfisi Februari 01, 2023.
Wakati akitoa salamu ameitaka idara ya Mahakama kuendelea kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya taratibu za kufuata wanapotaka kufika Mahakamani kwani kuna baadhi ya Wananchi wanahofia kufika mahakamani kupata haki zao kwa kuhofia tu kwamba wanaweza kufika wakageuziwa kibao na kuwekwa ndani.
Ameendelea kusema kuwa mahakama inayo wajibu wa kuendelea kuwaelimisha wananchi kwa vipindi mbalimbali kupitia vyombo ya habari na mitandao ya kijamii kwani wananchi watakapokuwa na Elimu ya kutosha watakuwa na uelewa kuwa mahakamani ni sehemu ya amani na inayosaidia wananchi.
Aidha ameitaka mahakama kupunguza muda wa kusikiliza kesi ambazo ziko mahakamani bali wajikite katika kutafuta namna ya kusikiliza kesi hizo na kuokoa muda wa kuzisikiliza ili kuendelea kufanya majukumu mengine ya kimaendeleo.
Vilevile ameitaka idara ya Mahakama kuepuka na kujihusisha na vitendo vya rushwa na amewataka Mahakimu pamoja na Watendaji wote kwenye muhimili wa Mahakama kuzingatia misingi ya maadili ya kazi ili waweze kutenda haki kwa Wananchi.
Kwa upande mwingine amevielekeza vyombo vya Usalama na taasisi zingine kama TRA, TAKUKURU, Polisi na Uhamiaji kuendelea kutenda haki kwa Wananchi na kuzuia wale wanaotumia nafasi kuzulumu haki za wanyonge na kuwapatia haki wale wenye nguvu za kifedha, lakini pia wasiruhusu wale wasio na mamlaka kukosa haki zao na kuwapatia wale wenye mamlaka. kwa kuzingatia hayo watakuwa wanatenda haki kwa wananchi , hivyo Wananchi watakuwa na uelewa mzuri kwa kuwa wanatenda haki.
Naye Hakimu mfawidhi Wilaya ya Kakonko Mhe.Ambilike Kyamba ameeleza katika maadhimisho ya mwaka huu 2023 ya wiki ya Sheria Mahakama kwa kushirkiana na Takukuru, Jeshi la polisi, Uhamiaji na Ustawi wa jamii wamefanikiwa kutoa Elimu ya Sheria kupitia mada mbalimbali katika Shule ya Sekondari Kanyonza, Donnybrook, Kakonko Sekondari, Kakonko wasichana, Muhange Sekondari na Kabare senta. Aidha Mahakama imefanikiwa kutoa Elimu kwa wajumbe wa baraza la kata la Kasanda na Kanyonza, hivyo Wananchi wengi wameelimishwa kuhusu mambo muhimu ya kisheria.
Pia Mahakama imeshiriki katika vipindi ya Radio kwizera kutoa Elimu na kuwasaidia Wananchi kuendelea kufaidika na Elimu ya Sheria.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu kwani ni wajibu wa mahakama na wadau.”
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa