Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndaki Stephano Mhuli amelipongeza shirika la Plan International kupitia mradi wa KAGIS (Keeping Adoloscent Girls in School) linalofanya kazi katika Wilaya ya Kakonko kwa kuendelea kutoa mchango wao ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu katika mazingira salama.
Amesema hayo ofisini kwake leo Alhamisi Mei 04, 2023 baada ya kuwapokea wawakilishi wa Shirika la ‘Plan International’ waliofika ili kutoa mrejesho wa miradi wanayoitekeleza ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Mkurugenzi Ndaki ameeleza kuwa shirika la Plan International limejenga vyoo na kuweka chumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika kata 03 ambazo ni Kasanda, Kiziguzigu na Gwanumpu.
Aidha shirika limetoa taulo za kike zaidi ya 1700 kwa mwaka 2022 katika shule za msingi na Sekondari kwa wanafunzi wa kike ili waweze kujikimu na kuendelea na masomo.
Mkurugenzi Mtendaji ameongeza kuwa Shirika limewafundisha watoto wa kike namna ya kutengeneza taulo za kike wao wenyewe kwenye mazingira yao na njia za kutunza na kuweza kuzitumia tena.
“Kwa hiyo tunawapongeza kwa namna ya pekee ambao wameendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali ya Serikali yetu ya awamu ya sita ili kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma bora”, Alisema Mkurugenzi Mtendaji.
Aidha Mkurugenzi Ndaki ameeleza kuwa Shirika limegawa baiskeli zaidi ya 100 kwa wanafunzi wa kike wa Sekondari ambao wanatoka umbali mrefu kutoka nyumbani kuelekea shuleni hivyo kuwasaidia wanafunzi kufika mapema shuleni na kuokoa muda wa kutembea na kuwapa fursa kupata elimu bora zaidi.
Aidha shirika limetoa vocha 350 kwa Wanafunzi wa shule za msingi hivyo kuwasaidia watoto kupata sare za shule, vitabu, viatu na vifaa mbalimbali vya kujifunzia.
“Elimu inayotolewa inawahamasisha watoto wapende shule na kukemea utoro kwa watoto na kitendo cha baadhi ya wazazi kutopenda elimu”, Aliongeza Mkurugenzi Ndaki.
Kwa upande wa miradi, Mkurugenzi Ndaki amewapongeza shirika la ‘Plan International’ kwa kutumia mfumo wa force akaunti hivyo kutekeleza miradi ya ujenzi kwa gharama nafuu na kutoa ajira wakazi wa maeneo husika hivyo kuendana na falsafa ya Serikali ya kutumia mfumo wa force akaunti.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa