Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kakonko kupitia program ya TAKURURU rafiki imeanza kutatua kero za Wananchi ikiwemo kero ya maji katika kata tatu za Kanyonza, Gwarama na Nyamtukuza kati ya kata 13 zilizopo.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kakonko Ladislaus Ibrahim ameeleza hayo wakati akitoa elimu kuhusu rushwa kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Halmashauri alipowatembelea leo Jumatatu Mei 8,2023 wakati wa kikao cha asubuhi ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji.
Ladislaus Ibrahim ameeleza kuwa TAKUKURU rafiki ni program ambayo imeanzishwa na Takukuru na lengo lake kuu ni kushirikiana na wadau kutatua kero katika ngazi ya kata kwani zile kero ambazo zinaachwa bila kutatuliwa zinaweza zikazaa vitendo vya rushwa au zikakwamisha utoaji wa huduma na miradi ya maendeleo.
“Kupitia programu hii ya TAKUKURU rafiki matokeo yameanza kuonekana kwa sababu kuna maeneo ambayo mtandao wa maji ulikuwa haujafika kwa sasa umepelekwa na huduma zimeanza kuboreka”, Alisema Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kakonko.
Akieleza kuhusu Elimu aliyoitoa kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo Bwana Ladislaus Ibrahim ameeleza kuwa lengo ni wakuu wa divisheni na Vitengo kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na amewaelimisha kuhusiana na usimamizi wa miradi ya maendeleo huku akitoa wito kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, Kanuni na taratibu na kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Program ya TAKUKURU rafiki inalenga kushirikisha wananchi kuzuia makosa ya rushwa kutokana na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 ambayo imeainisha makosa ya rushwa 24 na inaendeshwa ngazi ya kata na kujadiliwa na ikishindikana kero zinapelekwa ngazi ya Wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa