Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wananchi wa Wilaya ya Kakonko kuendelea kutunza Miundombinu ya Afya inayojengwa na Serikali ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Rais Samia amesema hayo siku ya Jumapili tarehe 16 Oktoba, 2022 wakati alipokuwa akifungua Hospitali ya Wilaya ya Kakonko iliyopo kijiji cha Itumbiko Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma iliyogharimu billioni 2.9.
‘’Wito wangu kwenu ni kutunza mali yenu, hii si mali ya Serikali, jitahidini kutunza Hospitali yenu iwahudumie leo, kesho na kesho kutwa.” Alisema Rais Samia.
Aidha Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuleta vifaa vya vipimo vyote ambavyo Mwanadamu akiumwa anatakiwa kupimwa kwani baadhi ya vifaa vipo lakini bado vingine havipo, hivyo Serikali itahakikisha inaleta vifaa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Hospitali ya Wilaya iliyofunguliwa ina jumla ya majengo nane ambayo ni jengo la kuwahudumia wagonjwa wa nje (OPD), Jengo la mionzi, Maabara, Jengo la dharura (EMD), Wodi ya mama na Mtoto (Maternity Ward), Jengo la dawa (Pharmacy), Jengo la kufulia na Nyumba za Watumishi 3 in 1.
Mbali na hivyo Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake wilayani Kakonko alizindua Mradi wa Maji Kakonko- Kiziguzigu uliopo eneo la Kanyamfisi, Ufunguzi wa barabara ya Kabingo- Nyakanazi km 50 iliyojengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami, pia alizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kihogazi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa