Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amewataka Viongozi kushirikiana na jeshi la polisi ili kuhakikisha uhalifu unaondoka huku akiwasisitiza viongozi wa dini kuwaambia waumini wao kufuata sheria na taratibu za Serikali pamoja na kuzingatia Imani zao.
Kamanda Makungu ameyasema hayo alipofanya kikao na kukutana na Viongozi mbalimbali akiwemo Kaimu Katibu Tawala, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Viongozi wa wa Jeshi la Polisi ngazi ya Wilaya na Vituo, Jeshi la akiba, Watendaji wa Kata na Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji na kamati ya maridhiano ambayo imehusisha Viongozi mbalimbali wa madhehebu ya kikiristo pamoja na waislamu.
Akizungumza katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Jumanne Aprili 02, 2024 Kamanda Makungu ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria namba 07 ya Serikali za Mitaa na vifungu vyake, Viongozi wanapaswa kuhakikisha usalama upo kwa Wananchi pamoja na mali zao.
Hata hivyo amesisitiza kuwa Wananchi wanapaswa kufuata sheria na maelekezo ya Serikali na endapo wanajitokeza watu wakorofi, vikao vifanyike ili kuwajadili na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Ninyi wote ni watekelezaji na wasimamizi wa sheria huko hakikisheni wananchi wanatii katiba na sheria ya nchi”, ameeleza kamanda Makungu.
Aidha Kamanda Makungu ameeleza kuhusu suala la wahamiaji haramu hususani katika Mkoa wa Kigoma ambao unapakana na nchi jirani ya Congo, Rwanda na Burundi kuwa wahamiaji wanatakiwa kuingia Tanzania kwa kufuata taratibu za nchi.
Kamanda makungu ameeleza kuwa raia yeyote wa Burundi au nchi nyingine anayekuja Tanzania anatakiwa awe na kibali maalum kutoka kwao. Na akifika Tanzania mfano anakuja kutafuta kibarua cha kulima au kufanya kazi akifika kwa Mwananchi au mwenyeji wake anatakiwa kupelekwa Mwenyekiti wa Kijiji au kitongoji ili kukaguliwa iwapo ana vibali.
Baada ya hapo anatakiwa apelekwe kwa Afisa Uhamiaji ili kupewa utaratibu wa kukaa naye kisheria na siku anataka kuondoka anatakiwa apelekwe kwa Mwenyekiti wa Kijiji au kitongoji kuona iwapo ana madai au amefuata taratibu zote.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma ameeleza viongozi wamepewa maeneo ya utawala kuyaongoza na kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ili anashangazwa anapofika sehemu na kuwauliza viongozi kuhusu taarifa za wahamiaji haramu na wao kusema hawajui hivyo kuhoji nani aulizwe sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli amemshukuru Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma kwa kufanya ziara Wilayani Kakonko na kueleza kuwa wapokea maelekezo na watafanyia kazi kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa