Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania na kushika kasi mwezi Januari 2024, madhara yamekuwa yakijitokeza kwa Wananchi ikiwemo nyumba kubomoka, mazao kuharibika, maeneo ya biashara kuathirikia na baadhi ya watu kupata majeraha na vifo hivyo kuleta maafa kwa jamii.
Serikali ya Tanzania imeandaa mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa maafa (2022-2027) ikidhamiria kulinda maisha ya watu na mali zao kutokana na maafa.
Akitoa dibaji katika mkakati wa Taifa wa usimamizi wa maafa (2022-2027) Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano waTanzania ameeleza kuwa Mkakati huu umeandaliwa kwa kuelewa kwamba mafanikio ya mipango yote ya maendeleo yanahitaji kulindwa dhidi ya madhara ya matukio ya maafa.
Hivyo Mkakati umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, Mpango Elekezi wa muda Mrefu 2011/12-2025/26), Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na sera, mikakati na mipango mbalimbali ya kisekta. Aidha, mkakati unawiana na mifumo ya kikanda na kimataifa inyohusu usimamizi wa maafa kama vile mkakati wa Sendai wa kupunguza hatari za Maafa 2015-2030, Malengo ya Maendeleo Endelevu, Mkataba wa Afrika wa kupunguza hatari za Maafa.
Kwa mujibu wa mkakati wa Taifa wa usimamizi wa maafa (2022-2027) maafa maana yake ni madhara yanayotokana na janga ambayo yanahusisha uharibifu wa mfumo wa kawaida katika jamii, kusababisha vifo, majeruhi, madhara ya kisaikolojia, upotevu au uharibifu wa mali, mifumo mbalimbali ya kiteknolojia na huduma za kiuchumi na kijamii au mazingira kwa kiwango chochote ambapo jamii iliyoathirika haiwezi kukabili kwa kutumia rasilimali zake bila msaada kutoka nje ya jamii hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Shirika la Chakula duniani (FAO) wameandaa na kutoa mafunzo Mkoani Kigoma kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Kakonko kwa Timu ya maafa ya Wataalam ili kueleza dhana ya Afya moja na kuwajengea uwezo.
Mafunzo hayo yamefanyika Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kuanzia Aprili 16, 2024 hadi Aprili 19, 2024 ikihusisha Wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waratibu wa maafa, Wataalam wa mifugo, Wataalam wa Mazingira, Wataalam wa maabara, Mratibu wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko (eIDSR FP), Watalam wa misitu na Maafisa mawasiliano.
Afya moja maana yake ni dhana inayotumika kuweka ushirikiano baina ya sekta zinazohusika na afya ya binadamu, wanyama na mazingira, ili kuimarisha uratibu na usimamizi katika utendaji na kupanga mikakati ya pamoja inayolenga kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na mlipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea na mazao ikiwemo madhara ya majanga yanayovuka mipaka na yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi, usugu wa madawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mmoja wa waratibu wa programu ya Afya moja Bi.Valentina Sanga wakati akitoa mafunzo hayo kwa washiriki ameeleza kuwa katika ngazi ya mkoa na Wilaya kumekuwa na majanga yanayojitokeza ambapo wataalam wamekuwa wakiyakabili majanga hayo kisekta hivyo dhana ya Afya moja inalenga kuunganisha nguvu ili majanga yanapojitokeza timu ya maafa ifanye kazi kwa pamoja hivyo kuunganisha utaalam, kuokoa muda na rasilimali fedha na kuweza kuifikia jamii kwa wakati na kupata mrejesho.
Mkoa wa Kigoma umekuwa ukiingiliana na nchi jirani za Kongo, Rwanda na Burundi hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na binadamu, wanyama na mimea.
Kwa mujibu wa ripoti ya Afya moja Tanzania kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Overview of one health platform in Tanzania), 60% ya magonjwa duniani yanatokana na wanyama. Aidha katika miongo mitatu imebainika kuwa 75% ya magonjwa ya binadamu yametokana na wanyama.
Wataalam walioshiriki kufundisha mada mbalimbali ni pamoja na Profesa Sharadhuli Kimera, Dr.Abubakar Shabani Hoza, Bi.Valentina Sanga, Justine Assenga, George Mrema, Salum Nyanga na Samwel Mngumi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa