Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mesha Mallasa amewahimizia wananchi kujitokeza kufanya biashara ya madini kwa uhalali ili kukuza uchumi wa mtu binafsi na nchi kwa ujumla na kutoa pongezi kwa Serikali kwa kutoa vifaa ambavyo vimewezesha soko la madini kuanza rasmi kazi ya kununua madini kuanzia tarehe 30.05.2022.
Akimkaribisha mfanyabiashara mpya wa madini (dealer) Injinia Hamenya Bichuro atakayekuwa ananunua madini kwenye Soko la dhahabu la Mkoa ambalo ofisi zake zipo Kakonko Col.Evance Mallasa amewahakikishia ulinzi wananchi na wafanyabiashara wa madini kwa ujumla wakati watakapokuwa wakifanya biashara ya madini.
“Serikali ya Mama Samia ni Serikali Sikivu, muda mrefu tulikuwa tumekosa vitendea kazi hivyo kutulazimu kufunga soko la awali, lakini kwa sasa Serikali imetoa vifaa, hivyo ‘dealer’ ataweza kufanya kazi vizuri, ‘Niwakaribishe wafanyabiashara wa Nchi Jirani Burundi, Rwanda na Congo kutumia fursa ya soko la dhahabu kuuza bidhaa zao za madini ya dhahabu”. Alisema Mwenyekiti wa kamati ya Usalama ya Wilaya Col.Mallasa.
Akimtambulisha ‘dealer’ mpya wa madini, Mhandisi kutoka Ofisi ya Madini Kigoma Bwana Orani Williad Mwashambwa amesisitiza Mfanyabiashara huyo ni kama mmea hivyo kuomba alindwe ili kuzuia mianya yote ya utoroshwaji wa Madini katika Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma ili madini yote yapelekwe Sokoni na kununuliwa kwa Uhuru kupitia soko la dhahabu lililopo Wilayani Kakonko.
Naye Mkaguzi Msaidizi wa Madini ambaye ndiye msimamizi wa Soko la Dhahabu Wilaya ya Kakonko Bwana Ishengoma Deogratius alieleza kuwa Soko la Dhahabu lilisimama kidogo kutokana na changamoto ya mashine ambapo hapo mwanzo walikuwa wakitumia vifaa vya ‘dealer’ yaani mfanyabiashara wa madini ambaye anaweka mtaji wake katika dhahabu kisha kununua dhahabu zinazoletwa na wafanyabishara ambapo baadaye aliondoka hivyo soko hilo kufungwa kwa miezi 10. Hivyo Ofisi ya Madini Waliamua kuomba Mashine hiyo na walifanikiwa kupata.
“Mpaka sasa ‘dealer’ amekata leseni na shughuli zimeanza rasmi tarehe 30/05/2022. Aidha mizigo yote ya Dhahabu katika Mkoa wote wa Kigoma pamoja na Nchi Jirani za Burundi, Rwanda na Congo zitakua zinauzwa katika Soko la Dhahabu Wilayani kakonko”. Alieleza bwana Ishengoma.
Tukio la ufunguzi rasmi wa soko la Kakonko baada ya kumpata mfanyabiashara mpya atakayekuwa ananunua madini limefanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kisha ukaguzi kufanyika katika Jengo la Soko la madini ya dhahabu la Mkoa lililopo Wilayani Kakonko na kushuhudiwa na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Buyungu Mhe.Aloyce Kamamba, Magreth Manamba fundi sanifu kutoka ofisi ya madini ya Mkoa wa Kigoma na Bwana Riud Bihurumba Mhasibu kutoka ofisi ya Madini ya Mkoa.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa