Timu inayosimamia mradi wa BOOST Wilayani Kakonko imefanya zoezi la kukagua na kutambua maeneo ya ujenzi wa Shule mbili (2) Mpya za Msingi, vyumba vya madarasa (20), Madarasa mawili (2) ya Mfano ya Elimu ya Awali, Nyumba Moja ya mwalimu na Matundu 15 ya vyoo kwa gharama ya Tshs.1,457,800,000 (Billioni Moja Millioni mia nne hamsini na saba na laki nane) kupitia Mradi wa BOOST.
Akiongoza timu hiyo Mratibu wa Mradi, Ndugu Erick Kudra ambae ni Afisa Elimu Msingi Vifaa na Takwimu akiambatana na Mhandisi wa Ujenzi, Afisa Mipango na Takwimu, Mthibiti ubora wa Shule, Afisa Usafi na Mazingira, Afisa Maendeleo ya Jamii, Afisa Ustawi wa Jamii pamoja na wajumbe wa kamati za ujenzi katika Shule husika wamekagua na kutambua maeneo ya ujenzi huo mwishoni mwa mwezi Aprili, 2023.
Shule hizo mbili (2) Mpya za Msingi zenye mkondo mmoja zitajengwa katika kata 2 ambazo ni Kata ya Kasanda Kijiji cha kazilamihunda na ujenzi utagharimu kiasi cha Fedha Tshs.361,500,000 na Shule ya Pili itajengwa katika Kata ya Nyamtukuza kijiji cha Nyamtukuza na ujenzi utagharimu kiasi cha fedha Tshs.361,500,000.
Aidha kutakuwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa (20) katika Shule ya Msingi Gwarama vyumba (4), Shule ya Msingi Bukirilo vyumba (4) , Shule ya Msingi Kigarama vyumba( 4), Shule ya Msingi Nyamwironge vyumba (4) na Shule ya Msingi Kavungwe vyumba (4) ambavyo vitagharimu jumla ya Fedha Tshs.520,000,000.
Vilevile kutakuwa na ujenzi wa Madarasa mawili (2) ya Mfano ya Elimu ya Awali katika Kata ya Gwarama Shule ya Msingi Gwarama na ujenzi utagharimu kiasi cha fedha Tshs.71, 800,000 na ujenzi wa Nyumba Moja ya mwalimu katika Shule ya Msingi Nyakivyiru utakaogharimu kiasi cha Fedha Tshs.110, 000.000.
Halikadhalika mradi wa BOOST utajenga Matundu ya Vyoo (15) vitakavyogharimu kiasi cha Fedha Tshs.33, 000,000, katika Shule ya Msingi Gwarama Matundu (3), Shule ya Msingi Bukirilo Matundu (3), Shule ya Msingi Kigarama Matundu (3), Shule ya Msingi Nyamwironge Matundu (3), na Shule ya Msingi Kavungwe Matundu (3).
Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2023. Mradi wa BOOST unatekelezwa kwa miaka 05 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026.
Utekelezaji wa mradi wa BOOST unatarajia kuboresha kiwango cha elimu na kutoa fursa za upatikanaji wa Elimu kwa Watoto wa elimu ya awali na msingi sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi Tanzania bara.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa