Halmashauri ya Wilaya Kakonko imezindua zoezi la ugawaji wa vyandarua 126,971 kwa Wananchi bila malipo lengo ikiwa kupunguza maambukizi ya malaria ambapo katika kipindi cha miaka mitatu maambukizi yamepanda kutoka 32% hadi kufikia 38.7%.
Sophia Ndembeto Ndalagura, Mratibu wa Malaria Wilaya ya Kakonko ameeleza kuwa wamefanya uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua 126,971 bila malipo kwa wananchi katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri leo Jumanne 3 Mei, 2025.
Dr.Sophia ameongeza kuwa maambukizi yameongezeka Wilayani Kakonko katika kipindi cha miaka 03 kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 ambapo maambukizi yamepanda kutoka 32% kwa mwaka 2022, 38.5% kwa mwaka 2024 na kuanzia Januari hadi Aprili 2025 maambukizi yamefikia 38.7%.
Mratibu wa Malaria amefafanua kuwa afua mbalimbali zinatumika katika kupunguza maambukizi ya malaria ikiwemo kutumia vyandarua vyenye dawa ili kupunguza hali ya maambukizi katika Wilaya ya Kakonko.
“Mwitikio wa wananchi upo chanya kwani wamefurahi kupata vyandarua kutoka kwa Rais Samia bila malipo”, alisema, Dr.Sophia.
Shukuru Abubakari Kisimba, mkazi wa Kakonko ameeleza kuwa wamefika kwa ajili ya kupata elimu ya matumizi ya vyandarua na kuhudhuria uzinduzi wakilenga kuepuka maambukizi ya malaria kwa kutumia vyandarua vyenye dawa.
Shukuru ameongeza kuwa, wamepanga kutumia mbinu walizoelekezwa ya kuzuia maji yaliyotuama kwani yanatengeneza mazalia pamoja na uondoaji wa vichaka katika mazingira wanayoishi.
Annastazia Kimatuzi Chiza, mkazi wa Kakonko na mnufaika wa vyandarua vyenye dawa bila malipo ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia vyandarua ili kuepuka kuugua malaria na kumwomba mheshimiwa Rais aendelee kuwajali na kuwakumbuka wana kakonko kwani yeye ni mama mwema ambaye amesaidia kukomboa wanawake na watoto ili wasiugue malaria.
Vyandarua 126,971vinategemewa kugawiwa kwa Wananchi katika kata 13, tarafa 03, na Vijiji 44 vilivyopo Wilayani Kakonko hivyo kupunguza maambukizi ya malaria.
Kauli mbiu, “Malaria inatokomezwa na sisi, wekeza chukua hatua, ziro Malaria inaanza na Mimi”.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa