Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma amewasisitiza Waalimu wa Shule za Msingi kuendelea kutoa Elimu juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia katika makundi yote hasa kwa jamii inayo wazunguka kwani kumekuwa na matukio mbalimbali yanayotokea katika Jamii na Shuleni.
Akiwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dr.Jesca Lebba katika ziara ya Kamati ya kutokomeza ukatili kwa Mtoto na Wanawake ya Mkoa iliyofanyika tarehe 07 Februari, 2023 Wilayani Kakonko ambapo alifanikiwa kufika katika Shule ya Msingi Maendeleo na kukutana na Wanafunzi waliojiunga na clabu ya juu ambayo ilianzishwa kwa lengo la kuimalisha Amani, Upendo, Ushirikiano na Kupinga Vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa Dr.Lebba amewaomba Wanafunzi wa Shule ya Msingi Maendeleo wasiogope kutoa taarifa pindi watakapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusisitiza waendelee kuhamasisha na kutoa Elimu kwa wazazi na jamii kwani wanaamini kupitia wao wakielimishwa itakuwa rahisi kufikisha ujumbe kwa Wazazi na jamii kwa Ujumla.
Dr.Lebba ameendelea kusema Vitendo vya ukatili vina madhara makubwa kwani kitendo ambacho anaweza kufanyiwa mtoto kitamuathiri maisha yake yote kwani kuna magonjwa mengi yanayoweza kujitokeza hivyo wajitahidi kuzuia vitendo hivyo na kutoa taarifa mapema.
“Tuendelee kubainisha hivi vitendo bila kuogopa na kuchukua hatua, tuna mahakama kwa ajili ya haki lakini pia tunaamini njia nzuri ni kuzuia ili vitendo visijitokeze”, Alisema Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa.
Hata hivyo Dr.Jesca amewasisitiza Waalimu kujitahidi kufungua sanduku la maoni mara kwa mara ikiwezekana kila siku kwani itasaidia kujua changamoto zinazowakabili wanafunzi ili waweze kuzitatua kwa wakati.
Dr.Jesca amewapongeza Waalimu kwa kuanzisha Elimu ya kujitegemea kwani itawajenga wanafunzi wasitegemee kuajiriwa kwani ukatili mwingi unajitokeza kutokana na suala la umasikini katika jamii. Hivyo wakiwajenga mapema itakuwa ni sehemu ya wao kuja kuwa na uchumi mzuri pia itawasaidia kutatua matatizo yote yanayotokea katika Jamii.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Maendeleo Mwalimu Samsoni Sike amesema kuwa wataendelea kuwaelimisha Wanafunzi juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na ukiukaji wa haki za Mtoto pia watakuwa na mashuhuda shuleni katika kupinga ukatili wa kijinsia.
“Sisi tuko mstari wa mbele ndio maana mnaona vijana wanajitambua na kujua dhana ya ukatili wa kijinsia na majukumu yao wanayafahamu”, Alisema Mwalimu Mkuu.
Mwalimu Sike aliendelea kusema kupitia kikundi hicho wemekuwa wakipata taarifa mbalimbali za ukatili unaotokea katika jamii hivyo wakipata taarifa kama hizo huwa wanasaidia watoto walioathirika na kitendo hicho kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali kama vile madaftari, sare za shule na chakula. Hivyo amewaomba kuendelea kusisitiza katika shule mbalimbali waweze kuwa na makundi ikiwezekana kila Shule wawe na makundi kwani itasaidia kupata habari mbalimbali zitakazowasaidia watoto kiakili, kimakuzi na kimalezi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa