Walimu 36 na wazazi 114 kutoka kata 13 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma wameshiriki Mafunzo ya uhamasishaji wa somo la Sayansi, Hisabati na Teknolojia kwa lengo la kuongeza ufaulu na kumfanya mtoto wa kike aweze kusoma na kupenda masomo hayo.
Walimu hao 36 wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati pamoja na wazazi 114 wenye ushawishi katika maeneo wanayotoka wameshiriki mafunzo hayo kwa ufadhili wa shirika la UNICEF katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri Machi 13 hadi 14, 2024.
Akifungua mafunzo hayo, Christopher Bukombe, Afisa Elimu Sekondari amewahimiza washiriki wa mafunzo kukaa na watoto wao wa kike na kuwahimiza kupenda masomo ya sayansi ili kufanya vizuri na kuondoa dhana potofu kuwa mtoto wa kiume pekee ndio anaweza masomo hayo.
Octavian Mgaya, kutoka taasisi ya FAWE Tanzania (Forum for African Women Educationalists) na mwezeshaji wa kitaifa kuhusiana na afua mbalimbali zinazosaidia maendeleo ya elimu hasa kwa wasichana ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wazazi na walimu ili wawe sehemu ya uhamasishaji kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya kwa watoto wa kike ili kuyapenda na kusoma masomo ya sayansi.
Mwezeshaji Mgaya amewaomba washiriki wa mafunzo kwenda kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na mtazamo hasi kwamba mtoto wa kike hawezi kusoma masomo ya sayansi na badala yake wawe sehemu ya kuwafanya watoto wa kike kupenda masomo hayo.
Bi.Christabel Alfani, Afisa Elimu kata Manispaa ya Iringa ambaye ni mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo, alieleza kuwa kutokana na ufaulu mdogo Serikali kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF walijadili namna gani ya kumwezesha mtoto wa kike aweze kufaulu masomo hayo na kuyapenda hivyo kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kuleta mbinu na dhana mbalimbali zitakazotumiwa katika kumwezesha mtoto wa kike kuongeza ufaulu wa masomo ya sayansi.
“Lengo la Serikali na UNICEF tutengeneze wazazi mashujaa wenye ushawishi ili waende wakashawishi na wazazi wengine wahamasishe watoto wetu wa kike waweze kupenda masomo”, alieleza Bi Christabel.
Wilfredy Kayonza, mmoja wa wazazi walioshiriki mafunzo, amewapongeza wadau wanaosimamia mafunzo hayo kwani yanaonyesha kuwajenga hivyo ameahidi kwenda kuyafanyia kazi mafunzo aliyoyapata kwa kuwapa elimu wazazi wenzake ili waweze kuhamamsisha watoto wa kike kupenda na kusoma masomo ya sayansi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa