Maafisa Elimu Kata 13 pamoja na walimu wakuu 69 wa shule za msingi wilayani Kakonko wamepatiwa mafunzo ya Jumuiya za ujifunzaji (JEZEKE) yatakayowawezesha kujengeana uwezo wenyewe kwa wenyewe na kuongeza umahiri wa ufundishaji.
Akifunga Mafunzo hayo, Afisa Elimu Msingi Wilaya ya kakonko, Bi.Isabella Mwakabonga ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uwezo wa walimu kufundisha kwa kupeana ujuzi wa ufundishaji wa masomo mbalimbali na kuweka mvuto kwa baadhi ya walimu kupenda kufundisha masomo mengine kutokana na ushuhuda wanaopata kwa walimu wengine kupitia jumuiya za ujifunzaji.
Afisa Elimu Msingi amongeza kuwa TAMISEMI kupitia mradi wa shule bora wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu kupitia (JEZEKE) ambapo jumuiya hizi zitapunguza changamoto za ufundishaji kwa baadhi ya masomo.
Akitoa ufafanuzi wa namna jumuiya hizo zinavyoendeshwa, Bi.Mwakabonga ameeleza kuwa walimu watakuwa wanakutana siku ya Ijumaa kupeana uzoefu na watatumia muda wa chai wakati wa siku za kawaida kwani jumuiya hizi hazichukui muda mrefu kwani ni endelevu hivyo kuwa moja ya jukumu katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, mwalimu Peter Mathias Mvuzwa, Afisa Elimu kata ya Muhange ameeleza kuwa zipo jumuiya mbalimbali za kujifunza ikiwemo walimu, walimu wakuu na maafisa elimu kata hivyo wamefika kujifunza namna ya kuanzisha jumuiya za ujifunzaji zitakazounganisha walimu wakuu na maafisa Elimu kata.
Ameongeza kuwa jumuiya hizi za walimu wakuu na maafisa elimu kata inakuwa na idadi ya walimu wakuu 10 -15 na maafisa elimu kata 2-3 ambazo zinalenga kuimarisha uwezo wa kila kiongozi hasa ngazi ya shule na kata kusimamia zoezi la ufundishaji na ujifunzaji ili kuleta ufanisi katika shule zao.
Mafunzo haya yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 21-23, Januari, 2025 katika shule ya msingi Kakonko ambapo jumuiya 06 za walimu wakuu na maafisa elimu kata zimeundwa katika Wilaya ya Kakonko na kushirikisha walimu wakuu 69, Maafisa elimu kata 13 na maafisa kutoka ngazi ya Wilaya 04.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa