Kuna usemi usemao ‘disability is not inability’ kwa tafsiri isiyo rasmi ina maana kuwa na ulemavu siyo kukosa uwezo wa kutenda jambo. Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha ulemavu chache kati ya hizo ni ajali, magonjwa, na kurithi vinasamba. Katika halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kuna jumla ya shule za msingi 59. Kati ya shule hizo 44 ni shule zenye Watoto wenye mahitaji maalum wenye viwango vidogo vya ulemavu ambapo shule zinazotengeneza ujumuishi ni 39 na zenye vitengo ni 5.
Kwa sasa jumla ya Watoto waliosajiliwa na kupata ruzuku ya chakula kila mwezi ni Watoto 293 kwa wilaya nzima. Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa katika kipindi cha miaka 7 kulingana na hali ilivyokuwa tete siku zilizokwisha.
Kihistoria Kitengo cha Elimu maalum kakonko kilianza mwaka 2016 kikiwa na wanafunzi 8 ambapo wavulana walikuwa 6 na wasichana 8 wote wakiwa na ulemavu wa akili wakifundishwa na waalimu 2.
Mwaka 2017 idadi ya wanafunzi iliongezeka na kufikia wanafunzi 11, wavulana 9 na wasichana 2. Kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa uliokuwepo katika shule ya msingi Kakonko uongozi wa elimu Kakonko uliomba vyumba 2 vya madarasa na ofisi moja kutoka Kanisa la Katoliki Kakonko ili kuweza kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mwaka 2018 wanafunzi 8 walisajiliwa hivyo kuleta jumla ya wanafunzi 19. Wanafunzi walikuwa wanafundishwa lakini hawakuwa na fungu la chakula kutoka Serikali kuu. Halmashauri ililazimika kutumia mapato ya ndani kuwapatia chakula Watoto hao. Hatimaye mwezi Julai, 2018 Kitengo cha Watoto wenye mahitaji maalum kilianza kupata huduma ya chakula cha asubuhi na mchana kwa ruzuku kutoka Serikali kuu.
Mwaka 2020 Halmashauri iliongeza vyumba 3 vya madarasa hivyo kupelekea Wanafunzi waliokuwa wakisoma katika majengo ya shule yanayomilikiwa na Kanisa katoliki kuhamia shule ya msingi Kakonko hivyo shule ikawa na kitengo na kuwa shule yenye elimu jumuishi. Hadi sasa kitengo kina wanafunzi 43 wenye ulemavu tofauti tofauti ikiwemo Watoto wasiioona, walemavu wa miguu, macho Pamoja na Ngozi.
Rekodi iliyowekwa na Watoto wenye ulemavu kwenye michezo ni ya kupongezwa na haijafikiwa hata na Watoto wasio na ulemavu kwani 2021 katika mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa Watoto wenye ulemavu walipata vikombe viwili vya mshindi wa kwanza kwa riadha maalum na mpira wa goli. Aidha Katika timu ya mkoa iliyohusisha wanafunzi sita kutoka shule ya msingi Kakonko walipata medali 11 za dhahabu. Pia michuano ya ‘Special Olyimpics’ yaliyofanyika Mwanza mwaka 2021 shule ya msingi Kakonko ilitoa mshiriki mmoja ambaye alijinyakulia medali 2 za dhahabu na 1 ya shaba.
Mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa Wataalam na Wazazi ambapo kwa kiasi kikubwa kazi iliyofanyika ni kubadili mtizamo wa Wazazi wenye ulemavu ili kukubali changamoto wanazopitia Watoto wao wenye ulemavu hatimaye kuwatoa na kuwapa fursa ya kupata elimu. Ni kweli bado ipo kazi ya kufanya lakini kupitia jitihada za Serikali kwa kipindi cha miaka 7 tangu kitengo kianzishwe mafanikio chanya yamejitokeza katika shule ya msingi Kakonko na shule nyingine kufikia kuwa na shule 44 zinazojumuisha Watoto wenye mahitaji maalum. Ni wakati sasa jamii iwape nafasi Watoto wenye mahitaji maalum hususani kwenye taaluma na michezo ili kuibua vipaji na Wataalam ambao watakuwa ni tunu ya Taifa kwa siku zijazo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa