Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso amewasisitiza Wananchi wa Kijiji cha Chilambo katika kata ya Kasanda Wilayani Kakonko kulinda na kutunza miundo mbinu ya maji katika mradi wa maji aliouzindua ili kuondoa changamoto ya maji waliokuwa wakiipata.
Amesema hayo Julai 19, 2023 baada ya kuzindua mradi wa maji wa Kijiji cha Chilambo uliokamilika kwa asilimia 100% kwa gharama ya Tshs.873,790,739.13 ukihudumia wakazi 3562.
Aidha Waziri Aweso ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kumpongeza Meneja wa RUWASA kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na Wataalam wengine wa maji na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na kujituma katika utendaji kazi wao.
Mbali na hayo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta mageuzi makubwa ndani ya Wizara ya maji na kuendelea kuwaletea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji na kuhakikisha adhima ya kumtua mama ndoo kichwani inatekelezwa na kutimia.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Buyungu Mhe.Aloyce Kamamba ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya maji kwa kuwaondolea adha wananchi ya upatikanaji wa maji kwani mji wa Kakonko ulikuwa na shida kubwa ya maji na wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata maji na kumuomba Waziri wa maji katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kutenga fedha zaidi ili kuendelea kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa ameishukuru Serikali na kueleza kuwa huduma ya upatikanaji wa maji ndani ya Wilaya ya Kakonko ni nzuri kwani mpaka sasa imefikia 80% ambapo Vijiji 38 kati ya 44 vimepata mtandao wa mabomba ya maji.
Vilevile amewasisitiza wananchi wote kutunza miundombinu yote ya maji pia kuendelea kutunza mabomba yote kwani wakitunza miundombinu vizuri itawasaidia kuendelea kupata maji kwa urahisi zaidi. Aidha amewaomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake kuhakikisha miundombinu inatunzwa.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa