Mkuu wa Mkoa Kigoma Mhe.Thobias Andengenye amewasisitiza Wananchi Mkoani Kigoma kujitokeza kupima Afya zao mara kwa mara, na wanapogundua wana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wasisite kufika vituo vya afya ili waanze dawa za kufubaza (ARV).
Amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyoadhimishwa Kimkoa Wilayani Kakonko katika uwanja wa Mwenge mwishoni mwa wiki siku ya alhamisi tarehe 01 Desemba 2022.
Katika hotuba yake amewasisitiza Wananchi kujiepusha na zinaa zinazochangia maambukizi makubwa ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuwahimiza wale watakaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wasisite kuwashawishi na wenza wao ili wakapime na kutambua hali ya afya zao.
“Ndugu zangu wanaume tuache tabia ya kupima kwa kutumia hadhi ya wake zetu waliopima, kwanza tujenge ustaarabu wa kuambatana na wake zetu kwenda kliniki wanapokuwa wajawazito, Kwa hiyo tupime tujue afya zetu kwa sababu kama tukianza kutumia hizi dawa ni vigumu kujua kama tuna changamoto yoyote ya maambukizi ya VVU”. alisema Andengeye.
Aidha Dr. Jesca Lebba, Mganga Mkuu wa Mkoa alitoa takwimu ya hali ya maambukizi ya VVU kwa Mkoa wa Kigoma kuanzia Januari hadi Oktoba 2022 kuwa yamepungua kwa asilimia 2.9 kutoka asilimia 3.4 hivyo jumla ya Wananchi waliogundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) ni [G1] elfu tatu mia nne na moja (3,401), kati ya Wananchi laki moja sabini na tatu mia saba kumi na tisa (173,719) waliopima.
Dr. Jesca aliendelea kusema kuwa katika Mkoa wa Kigoma kuna vituo 83 vya kutolea huduma ya virusi vya UKIMWI na vituo hivyo vyote vinafanya kazi. Aidha Mkoa una mpango wa kuongeza vituo vingine vya kutolea huduma. Hivyo wananchi waendelee kujitokeza kupima Virusi vya UKIMWI.
Japhet Jerome Mkazi wa Kakonko aliwashauri wanaume wasiogope kwa kuona aibu kwenda kituo cha afya na wenza wao kupima maana wanapojitambua kuwa wana maambukizi ya VVU watajipanga namna ya kuishi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa