Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amewataka Wananchi kumiliki Ardhi kwa kufuata taratibu na sheria ili kujiletea maendeleo.
Amesema hayo jana Mei 15,2024 Katika Kijiji cha Luhuru kitongoji cha Bwela Kata ya Muhange wakati wa ziara ya kusikiliza kero mbalimbali za Wananchi.
Aidha kanali Mallasa amewataka viongozi wa Taasisi za kidini kutotumia taasisi zao kuwakandamiza wananchi badala yake wafuate taratibu katika umiliki wa aridhi.
Katika ziara hiyo wananchi wa kitongoji cha Bwela, waliibua hoja ya kutakiwa kuachia maeneo ambayo wanaishi, kwa kile kinachodaiwa kuwa maeneo hayo yanamilikiwa na Kanisa katoliki parokia ya Muhange.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha kusikiliza kero za wananchi, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Luhuru, January Bonga, alieleza kuwa mgogoro huo umeibuka kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa Mwaka 2023 ambapo uongozi wa kanisa Katoliki, ulipita kukagua eneo hilo ambalo wananchi wanadai wamekuwa wakifanya shughuli zao tangu Mwaka 1993.
Naye Paroko wa Parokia ya Muhange Padre Emil Mateo, alieleza kuwa kanisa katoliki lilikuwa likimiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 100 tangu mwaka 1936.
Kwa upande wake Afisa Ardhi Danstan Kisaka, alieleza kuwa ofisi ya ardhi haina nyaraka yoyote inayoonesha kuwa eneo hilo linamilikiwa na kanisa katoliki.
Vilevile eneo hilo halijaendelezwa kwa muda mrefu jambo ambalo linaondoa uhalali kisheria wa umiliki wa kanisa katoliki.
Akihitimisha kikao hicho cha kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Kanali Mallasa amewataka wananchi, taasisi na mashirika binafsi kuzingatia Sheria ya ardhi katika kupata na kumiliki ardhi kisheria ili kuepuka migongano isiyokuwa na tija.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa