Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndugu Ndaki S. Mhuli amewahimiza Wananchi wa Kata ya Nyabibuye Wilayani Kakonko pamoja na Wananchi wa Nchi jirani ya Burundi kulitumia vizuri Soko ili waweze kunufaika.
Amesema hayo leo Machi 09, 2023 Wakati alipokaribishwa katika hafla fupi ya kufungua Soko la Ujirani Mwema la Nyabibuye lililopo Mpakani Mwa Burundi na Tanzania katika Kata ya Nyabibuye Wilaya ya Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji ameeleza kuwepo kwa Soko la ujirani Mwema baina ya Nchi jirani ya Burundi na Tanzania kutachochea kukua kwa uchumi wa Mwananchi wa Burundi na Tanzania pamoja na kukua kwa Uchumi wa Nchi zote Mbili.
Aidha amewasisitiza Wananchi wote wenye bidhaa kwa pande zote mbili za Burundi na Tanzania kuchangamkia fursa ya kufanya bishara katika soko hilo ili kujiongezea kipato.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji ameahidi kupatikana kwa umeme, maji, na kufanya marekebisho ya miundombinu ya milango ya vyoo vya Soko pamoja na barabara na mwisho amewaruhusu Wananchi wote wa Burundi na Tanzania ndani ya Mwezi mmoja kufanya biashara bila kulipa ushuru.
Amehitimisha kwa kusema Wananchi wote wa Burundi na Tanzania Sisi wote ni ndugu tusifanyiane matendo ya ukatili bali tupendane.
Fediriko Nzoyisaba Afisa Tarafa ya Mishiha iliyopo Nchini Burundi ameeleza amefurahishwa na kitendo cha kualikwa katika hafla fupi ya ufunguzi wa Soko hilo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika biashara ili kukuza uhusiano mzuri wa kibiashara na Nchi ya Tanzania.
Aidha Ndugu Fediriko Nzoyisaba ameeleza Tarafa ya Mishiha ilikua haina soko siku ya alhamisi hivyo amefurahi kusikia kwa sasa Wananchi wa Burundi watakua wakifanya biashara zao katika Soko la Ujirani Mwema la Nyabibuye na amewakaribisha Wananchi wa Tanzania kufika katika Masoko ya Mipakani ya Ujirani Mwema ya Burundi kufanya Biashara zao na hakutakua na kikwazo chochote cha kibiashara Wananchi wote watafanya bishara zao kwa amani.
OCD SSP Mohamed M.Mussa ametoa angalizo kwa Wananchi kutofumbia macho vitendo vya uhalifu katika soko hilo bali watoe taarifa za uhalifu kituo cha polisi na kwa viongozi wa Kata.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa