Mkuu wa Wilaya ya Kakonko kanali Evance Mesha Mallasa amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Gwanumpu wilaya ya Kakonko kwa lengo la kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati ya muwekezaji na Wananchi wa kata ya Gwanumpu.
Mgogoro huu wa ardhi umeibuka baada ya Uongozi wa Kijiji cha Bukirilo kumpatia mwekezaji ekari 50 kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa kisasa, ambapo hapo awali Serikali ya Kijiji ilitenga eneo hilo kwa ajili ya wafugaji.
Akieleza chanzo cha mgogoro huo Diwani wa Kata ya Gwanumpu Mhe. Toyi Butono alieleza kuwa chanzo cha mgogoro huo ni baada ya Wakulima kukuta mashamba yao yamewekewa bikoni na muwekezaji, hivyo wananchi kuhoji hatima ya maeneo yao ya kilimo.
Mhe. Toyi aliendelea kusema kuwa tangu awali eneo hilo lilikwisha tengwa kwa ajili ya wafugaji na si wakulima, bali kuna shida kubwa ya wananchi wa Kata ya Gwanumpu kukodisha mashamba kwa raia kutoka nchi jirani ya Burundi kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji hali inayopelekea kuibuka kwa migogoro ya ardhi.
Aidha, Mhe. Toyi aliwasisitiza Wananchi wa Kata ya Gwanumpu kuwa Wazalendo kwa Nchi yao kwa kuacha kukodisha mashamba kwa raia kutoka Burundi pamoja na kuacha kuingiza mifugo Nchini Tanzania kutoka Burundi kwa kuzingatia hayo hakutakuwa na changamoto ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Akihutubia katika Mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki Aprili 14, 2023, katika kijiji cha Bukirilo kilichopo katika Kata ya Gwanumpu Wilayani Kakonko, Kanali Mallasa alieleza kuwa “Hatutamani tuwe jamii ya wana Kakonko ambao tunafuga nyasi, nyasi hizi tumekaa nazo miaka mingi, tunataka haya maeneo yabadilike yawe sehemu za uwekezaji, sehemu ya kukuza uchumi wetu, Sehemu ambayo hata mdogo wetu ambae hajafanikiwa kwenda shule anajifunza kutoka kwa wenzake wanafanya kitu gani, sehemu ambayo watu wengine wanapata ajira, ndiyo hasa msingi ambao Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alituambia tuhakikishe maeneo yetu yanakuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.’’
Aidha Kanali Mallasa alisisitiza Wananchi kuendelea kutumia maeneo waliyotengewa na uongozi wa kijiji kwa matumizi ya kilimo na ufugaji bila kuingiliana ili kuepuka migogoro.
Vilevile alisisitiza Uongozi wa Vijiji kuhakikisha unatenga maeneo ya uwekezaji, kwani serikali imekwisha tenga fedha mahususi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji wa kilimo.
“Pochi la mama lipo wazi na fedha kwa sasa zipo na zinatawanywa kila Wilaya, sasa kwa sisi wana Kakonko hatuwezi kujitenga ni lazima tuwe na maeneo ya uwekezaji ili Serikali iweze kuleta fedha hizo kwa ajili ya uwekezaji wenye manufaa,’’ aliongeza Kanali Mallasa.
Aidha alieleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Inaendesha programu maalumu ijulikanayo kama “Build Better Tommorow” (BBT) ambapo programu hii imelenga kuwainua vijana kiuchumi ambao wanategemea shughuli za kilimo, programu hii imeanzishwa kwa kuzingatia asilimia kubwa ya wananchi nchini wanategemea shughuli za kilimo, ukilinganisha na asilimia ndogo ya wafanyakazi. hivyo amewaasa vijana kuchangamkia fursa hii adhimu ili kutuma maombi ya kujiunga na programu ya BBT, ambapo vijana watakaochaguliwa watapewa mafunzo kuhusu kilimo bora kwa muda wa miezi mitatu, baada ya mafunzo hayo watarejea katika maeneo yao na kupatiwa ardhi kiasi cha ekari 10 kwa kila kijana na serikali itawapatia hati miliki za maeneo hayo pamoja na kugharimia shughuli zote za uendeshaji wa kilimo.
Kwa upande Mwingine Kanali Mallasa alitoa rai kwa Wananchi kuwa makini na baadhi ya wanasiasa wanaowahamasisha kushiriki vitendo vya uvunjifu wa Amani ikiwemo kushiriki maandamano bila kufuata sheria, kwani viongozi hao wa kisiasa wanawapotosha wananchi kuwa aridhi yao imeporwa na kupewa muwekezaji. ‘’Hivi sasa tunaelekea kipindi cha uchaguzi Wananchi msitumike vibaya na wanasiasa,mkirubuniwa kuwa aridhi yenu imeporwa na uongozi wa kijiji na kupewa muwekezaji, niwaombe wananchi wote ambao maeneo yenu yamechukuliwa na akapewa muwekezaji, orodhesheni majina yenu na ukubwa wa maeneo yenu kupitia kwa Mtendaji wa Kata, yanifikie ofisini, nitatenga siku maalum kufika eneo husika na nitahakikisha kila mmoja anapata haki yake” alisema Kanali Mallasa.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria katika mkutano wa hadhara ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Afisa ardhi, Kamati ya Ulinzi na usalama na wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa