Wananchi wa Kata ya Nyamtukuza iliyopo Wilayani Kakonko kupitia diwani wao Mhe.Abdallah Magembe wameomba barabara ya kutoka Nyamtukuza kwenda Nyakiyobe ichongwe kwani barabara hiyo ikichongwa itakuwa rahisi kwa wananchi kupita na kusafirisha mazao yao bila changamoto kwani wananchi wengi wanapitia barabara hiyo.
Aidha Diwani Magembe amemuomba Meneja wa TARURA kushirikiana nae pale wanapomleta mkandarasi kwa ajili ya kufanya vipimo vya barabara kwani yeye anapata maswali mengi kutoka kwa Wananchi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo.
Diwani Magembe ameyesema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Usalama ya Wilaya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa kutembelea barabara mpya ya Nyamtukuza - Nyamwironge yenye urefu wa Kilometa 2.5 Februari 10, 2023 ambapo Mradi huo umegharimu Tshs.551,891,214,000/= (Milioni mia tano hamsini na moja, laki nane tisini na moja mia mbili kumi na nne).
Meneja TARURA Injinia Erasto Mlengela amesema kuwa wana mpango kufikia mwaka 2024 waweze kuunganisha barabara inayotokea Bwera kuja Nyamtukuza kuondoa changamoto kwa wananchi kwani watakapokutanisha barabara hiyo itakuwa rahisi kwa wananchi kufika Kakonko bila kutembea umbali mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amewaomba TARURA kuorodhesha changamoto zote zilizojitokeza na kumuonesha mkandarasi ili aweze kuzifanyia kazi pale ambapo kuna matatizo ili kazi iweze kumalizika kwa kiwango kizuri.
Mradi huo ulianzishwa mwaka 2021 na kumalizika tarehe 29.08.2022 na mradi ulitekelezwa kwa fedha za tozo mwaka wa Fedha 2021-2022 ikiwa chini ya kampuni ya Kosiga.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa