Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col. Evance Mallasa amewasisitiza wananchi wote wa Wilaya ya Kakonko kuhakikisha wanajitokeza kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya polio kwani chanjo hiyo ni muhimu kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane.
Amesema hayo leo Novemba 3, 2023 alipokuwa akizindua zoezi la utoaji wa chanjo ya polio awamu ya pili katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Wilayani Kakonko.
Kanali Mallasa amesema zoezi hilo linaenda nyumba kwa nyumba hivyo amewataka wananchi kuwepo majumbani ili kuhakikisha wanawapatia ushirikiano wahudumu wa afya pale wanapowafikia kwa ajili ya kutoa chanjo ili kuhakikisha zoezi hilo linaenda vizuri na kwa muda uliopangwa.
Kanali Mallasa amewapongeza wahudumu wa afya kwa kazi nzuri wanayoifanya na Wilaya itahakikisha inaendelea kutatua changomoto zote zitakazokuwa zinawakabili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli ameeleza kuwa Halmashauri imejipanga kuwafikia watoto wote na kuhakikisha wanapata chanjo kwani wataalamu wa Afya wamejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linaenda vizuri.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Dr.Getera Nyangi, ameeleza kuwa lengo la utoaji wa chanjo ya polio ni kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa polio katika Wilaya ya Kakonko na taifa kwa ujumla ambapo ameeleza mpaka sasa watoto elfu tatu mia tano (3,500) wameshapatiwa chanjo ikiwa lengo la Wilaya ni kuwafikia watoto elfu themanini na sita na tisini na mbili (86,092).
Ameendelea kusema kuwa mtoto mdogo yupo katika hatari kubwa katika kupata ugonjwa wa polio hivyo amewasisitiza wazazi kuhakikisha wanatoa ushirikiano na kujitokeza kuwapeleka watoto kupata chanjo hiyo.
Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Kakonko Planner Erasto, ameeleza kuwa zoezi hili linalofanyika kwa awamu ya pili linalenga kuhakikisha wanawakinga watoto wote dhidi ya ugojwa wa polio.
Pia Mratibu ameeleza kuwa wamepokea chanjo laki moja na elfu sita (106,000) ambapo kupitia chanjo hizo wanaamini zinaenda kuwafikia walengwa wote na kufikia lengo walilokusudia ndani ya Wilaya ya Kakonko.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa