Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amewasisitiza Wananchi kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa kata pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii ili kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na Watoto.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 29, 2023 katika Kijiji cha Chilambo kilichopo katika kata ya Kasanda Wilayani Kakonko, Kanali Mallasa amesema kuwa ukatili wa kijinsia unatokea katika jamii hivyo wazazi wanao wajibu wa kuwalinda watoto ili kudhibiti ukatili wa kijinsia kwa jamii.
Kanali Mallasa ameeleza kuwa kumekuwa na vishawishi vinavyofanywa na baadhi ya mashirika mbalimbali hasa kwa watoto wadogo na kuwaingiza kwenye vitendo viovu ambavyo ni kinyume na maadili ya kitanzania hivyo amewaomba wazazi kujitahidi kuwalinda watoto na kuwapatia huduma bora ya Elimu, kuhakikisha matumizi ya sheria yanafuatwa kwani itasaidia kutokomeza vitendo hivyo ndani ya Wilaya ya Kakonko na kuwa makini wanapoletewa misaada ya aina yoyote.
“Tusikae kimya tutoe taarifa mapema kwa viongozi wetu wa Kata pia tushirikiane wa pamoja kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii na Wilaya ya Kakonko kwa ujumla,” Alisema Kanali Mallasa.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kakonko, Mohamed Masoud, amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokea katika jamii na kuwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza ulinzi shirikishi pia amewaomba wazazi kutoa taarifa mapema pale watoto wao wanapobebeshwa ujauzito kwani kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia na atakayebainika amembebesha ujauzito mtoto wa kike hatua za kisheria zitachukuliwa.
Kwa upande wake Afisa Ustawi Bi.Epheta Msiga amewasisitiza wazazi kujitahidi kutoa maadili mema kwa Watoto wao na ikitokea mtoto amelawitiwa, amebakwa au kufanyiwa ukatili wa kijinsia ameomba wazazi kutoa taarifa mapema ili waweze kusaidiwa kwa wakati.
Aidha Bi.Epheta amewasisitiza vijana kutotumia simu kwaajili ya kuwaonyesha watoto vitu ambavyo haviendani na umri wao na badala yake wazitumie kwaajili ya mawasiliano.
Naye Diwani wa kata ya Kasanda, Mheshimiwa Dickson Barutwa amewashukuru Ustawi wa jamii kwa kuendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na kuwaomba waendelee kushirikiana kwa pamoja ili kutokomeza ukatili kwani wakifanya hivyo itasaidia jamii kuondokana na vitendo hivyo na kuwaomba wananchi wasikae kimya na badala yake watoe taarifa kwa viongozi ili kutokomeza ukatili kwa jamii.
Jenipha Kabugabuga mkazi wa Kijiji cha Chilambo ameiomba serikali kuendelea kushirikiana na wananchi kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwani watoto wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili hasa ubakaji hivyo elimu iendelee kutolewa zaidi kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa