Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mzava amewataka wananchi Wilayani Kakonko kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa kuzingatia kanuni za kiafya kwenye maeneo yao.
Bw. Mzava amezema hayo leo Jumamosi Septemba 21, 2024 akitoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru kwa wananchi wa kijiji cha Nyakayenzi Wilayani Kakonko ambapo amesema ugonjwa wa malaria unaendelea kusumbua kutokana na baadhi ya wananchi kutozingatia matumizi sahihi ya vyandarua pamoja na usafi wa mazingira yao.
Aidha amesema nia ya Serikali ni kuona wananchi wakiendelea kufanya shughuli zao wakiwa na afya nzuri hivyo ni vema wataalamu wa afya kuanzia ngazi za vijiji na kata wakaweka utaratibu wa kuwaelimisha wananchi juu ya njia za kujikinga na ugonjwa huo
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amesema kupitia mikusanyiko mbalimbali halmashauri itaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya njia za kujikinga na ugonjwa wa malaria sambamba na magonjwa mengine pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira hususani katika msimu wa mvua.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wilayani kakonko mkoani kigoma wameahidi kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa malaria na kuiomba Serikali kuongeza kasi ya usambazaji wa vyandarua ngazi zote.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa