Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Evance Mallasa amewasisitiza Wananchi wa Wilaya ya Kakonko kuepuka vitendo vya ukataji wa miti ovyo bila kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali ikiwemo uchomaji wa misitu kwa ajili ya shughuli za mbao na uchomaji wa Mkaa.
Amesema hayo wakati akizindua zoezi la upandaji wa miti katika eneo la Stendi ya Mabasi ya kisasa Kakonko Mjini leo Ijumaa tarehe 25/11/2022 na kutoa wito kwa viongozi wote kupanda miti katika maeneo yao. aliongeza kuwa Taasisi za Serikali, Binafsi, Taasisi za dini, Shule zote na Hospitali wapande miti katika maeneo yao na maeneo mengine yanayofaa kupandwa miti.
“Nataka nitumie fursa hii kutoa wito kwa Mwananchi wote wa Wilaya ya Kakonko kuanzia katika familia kila mmoja wetu ajitahidi kupanda miti katika eneo lake kwa ajili ya kuvuna mbao kuepuka janga la umasikini na kujipatia kipato,” alisema Mallasa.
Aidha ameeleza kuwa Wataalam wa TFS wameleta Mbegu nzuri zinazotumia muda mfupi kustawi takriban miaka 7. Hivyo Mwananchi yeyote ambae atabainika akifanya vitendo vya biashara ya miche badala ya kupanda katika eneo lake hatua za kisheria zitachukuliwa.
Aliongeza kuwa Wananchi wote ambao miti imepandwa katika maeneo yao ya barabara wanapaswa waitunze na kuihudumia kwa kuzungushia uzio ili miti hiyo isiharibiwe na wanyama.
Aidha Mkuu wa Wilaya alitoa rai kwa Wananchi wa Wilaya ya Kakonko kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji ili kuepuka kukosa mvua kwa muda mrefu pamoja na hewa safi.
Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi Wakala wa huduma za Misitu Wilaya ya Kakonko (TFS) Paschal Amosi Misita alieleza kuwa katika Wilaya ya Kakonko Mjini imepandwa Miti 522, lakini kwa Mwaka 2022/2023 wamepanga kupanda Miche ya Miti laki mbili (200,000).
Aliendelea kusema Miche hiyo ya Miti itagawiwa kwa Wananchi wote bure ili wakapande katika maeneo yao. Aidha alisisitiza wananchi watakaochukua miche ya Miti watafuatiliwa kuona kama wametekeleza agizo la Serikali la kupanda Miti kwani kumekuwa na tabia ya baadhi ya Wananchi kuchukua miti pasipo kupanda.
Farida Ismail, Mwananchi wa kata ya Kakonko ameeleza kuwa zoezi la upandaji miti amelipokea vizuri na ameahidi kuendelea kuwahamasisha Wananchi kupanda Miti na kuitunza. Uwepo wa miti unachangia upatikanaji wa Mvua na hali ya hewa nzuri. Hivyo anaishukuru ofisi ya Mkuu wa Wilaya na TFS kwa kuendesha zoezi la upandaji miti.
Issa Laurent, Mwananchi wa Kijiji cha Mbizi ameeleza anaushukuru Uongozi wa Wilaya kwa kuendelea kuhamasisha Wananchi kupanda miti katika maeneo yao. Kwa upande wake ameeleza kuwa amehamasika na zoezi hilo na kuahidi kwenda Hifadhi ya TFS kuchukua Miche ya Miti na kwenda kupanda. Kwani miti hiyo italeta manufaa kwa ajili ya kizazi cha baadae.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa