Kufuatia maadhimisho ya siku ya mwanamke kiwilaya yaliyofanyika Wilayani Kakonko Machi 7, 2024 katika kata ya Mugunzu, Wanawake wamelalamikia baadhi ya wanaume kutojishughulisha kusaidiana na wake zao badala yake wanatelekeza familia na kujikita kwenye starehe.
Akizungumzia changamoto hiyo kwa undani Bi.Mariam Sadala mkazi wa Kata ya Mugunzu ameeleza kuwa akina baba wamejikita sana kwenye ulevi na kurudi usiku hivyo kukosa muda wa kukaa na familia hususan wake zao ili kujadiliana namna ya kujenga familia.
Ameongeza kuwa akina mama wanajishughulisha sana na kutunza familia zao kwa muda mrefu na kwa nguvu.
Ameendelea kuongeza kuwa unakuta mama analima, anavuna na kuhifadhi mazao ndani kwa lengo la kupumzika angalau hata miezi miwili lakini inatokea baba hususan mlevi anachukua yale mazao bila kumshirikisha na kwenda kuyauza hivyo suala hili kuumiza sana akina mama wa Kijijini.
“Akina baba kwa kweli kama wanatusikia watusaidie, familia ni ya watu wawili siyo mtu mmoja, mwanamke hawezi akazaa akiwa peke yake, mwanamke anazaa akiwepo mwanaume hivyo kama wameweza kuzaa watunze familia zao”, ameeleza Bi.Sadala.
Diwani wa kata ya Katanga, Mhe.Ezekiel Bikata amekiri kuwa hilo linaloelezwa na akina mama lipo na kweli wamekuwa wakilalamika. Ameeleza kuwa tayari wameishauri Serikali ijaribu kuleta watu wa maendeleo ya jamii kukaa na hao watu.
Ametolea mfano kata yake ya Katanga ambayo ipo jirani na kata ya Mugunzu tayari wameletewa Afisa Maendeleo ya Jamii hivyo wamekuwa wakipokea migogoro ya mke na mume, mke analalamika kuwa anahangaika na familia peke yake, mume kazi yake ni kunywa pombe, akiamka anaamkia kwenye ulevi, hivyo amezungumza na Afisa maendeleo ya Jamii ili kuzungumza na akina mama na akina baba ili kuwepo na mabadiliko na utekelezaji umeanza.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko
Anuani ya Posta: P.O.BOX 3
Simu: +255(028) 2988881
Simu ya Mkononi: +255(028) 2988881
Barua Pepe: ded@kakonkodc.go.tz
Hatimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Haki zote zimehifadhiwa